Wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wawataka maseneta kutupilia mbali wazo la kuongezwa kwa madeni

Wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza wawataka maseneta kutupilia mbali wazo la kuongezwa kwa madeni

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wanaoegemea muungano wa Kenya Kwanza (KKA) wamewataka maseneta kutupilia mbali pendekezo la kuongezwa kwa kiwango cha fedha ambazo serikali inaweza kukopa kutoka hadi Sh9 trilioni hadi Sh10 trilioni.

Wakati huu Kenya imekopa jumla ya Sh8.4 trilioni ilhali kiwango cha juu zaidi ambacho serikali inaweza kukopa wakati huu ni Sh9 trilioni, ambacho kiliwekwa mnamo Oktoba 9, 2019 kupitia idhini ya Bunge la Kitaifa na Seneti.

Baadhi yao waliozungumza na Taifa Jumapili jana Jumamosi, Juni 18, 2022 katika mahojiano, kwa njia ya simu, walitaka maseneta watakaofanya kikao maalum Jumanne, Juni 21, 2022 kukataa pendekezo hilo kutoka kwa serikali kuu.

Wabunge, Kimani Ichungwa (Kikuyu), Didmus Barasa (Kimilili) na Robert Pukose (Endebess) walisema kuwa ongezeko la kiwango cha fedha ambazo Kenya inaweza kukopa linawekea vizazi vijavyo mzigo mzito.

“Ingawa bunge letu lilipitisha pendekezo hilo mnamo Juni 9, 2022, licha ya upinzani mkali kutoka kwetu sisi kama wafuasi wa Kenya Kwanza, nawaomba wenzetu katika seneti wasiidhinishe nyongeza ya kiwango cha mkopo hadi Sh10 trilioni kwani walipa ushuru watawekewa mzigo mzito wa kulipa madeni hayo,” akasema Bw Ichungwa, ambaye zamani alihudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti.

Kwa upande wake Bw Barasa alisema kuongezwa hatua hiyo itaikosesha serikali ijayo fedha za kutumia katika kuendesha shughuli zake kando na kufadhili miradi ya maendeleo.

“Ikiwa wakati huu jumla ya Sh1 trilioni kutoka bajeti ya kitaifa hutumika kulipia madeni ya kigeni, haswa kutoka China, hatungependa mzigo huu kuongezwa tena. Hii ndio maana nawataka maseneta kukataa pendekezo hilo,” akaeleza.

Dkt Pukose, ambaye ni tabibu katika nyanja ya upasuaji, alisema kwa kupunguzwa kwa mikopo ndiko kutawezesha kupatika kwa pesa za kupiga jeki sekta ya afya.

Mnamo Jumanne, Juni 21, 2022 maseneta watafanya kikao maalum kujadili na kupigia kura pendekeza la Wizara ya Fedha ya kutaka serikali iruhusiwe kukopa hadi Sh10 trilioni kufanikisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Mnamo Juni 9, Bunge la Kitaifa lilikubaliana na pendekezo hilo la Wizara ya Fedha katika kikao cha mwisho cha bunge hilo katika muhula wa bunge la 12.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya, wakiongozwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya.

Wabunge hao walifanya hivyo kwa kuifanyia marekebisho Kanuni ya Usimamizi wa Fedha za Umma katika Serikali ya Kitaifa ya 2015.

Kanuni hiyo ilichapishwa kama notisi ya kisheria ya 89 ya 2022.

“Kwa mujibu wa hitaji la Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM Act), Bunge hili linapitisha Kanuni ya Sheria hiyo ya 2022, kwa kuamuru kwamba deni la kitaifa halitazidi Sh10 trilioni,” hoja hiyo maalum ikasema.

Serikali ijayo itatarajiwa kutekeleza bajeti ya kima cha Sh3.3 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2022/23 unaoanza Julai 1, 2022. Bajeti hiyo ina pengo la Sh846 bilioni ambalo serikali inafaa kuliziba kwa kukopa humu nchini na nje.

Kwa kuwa wakati huu mzigo wa madeni ni Sh8.4 trilioni, ina maana kuwa serikali itaruhusiwa kukopa hadi Sh600 bilioni pekee. Kwa hivyo, kutakuwa na pengo lingine la Sh246 bilioni.

Wabunge wengine waliunga mkono hoja hiyo ni pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kanini Kega, Opiyo Wandayi (Ugunja), William Kamket (Tiaty) na Jeremiah Kioni (Ndaragua).

  • Tags

You can share this post!

Wizara imebana pesa za corona – Mkaguzi

Sadio Mane aendea mamilioni ya Bayern Munich

T L