Habari Mseto

Wabunge wa Pwani waomba waathiriwa wa mafuriko wasaidiwe

November 14th, 2019 1 min read

Na Charles Wasonga

WABUNGE wa Pwani wameitaka serikali ya kitaifa kutuma Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaidia wakazi wa eneo hilo ambao wameathirika na mafuriko kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa eneo hilo wakati huu.

Wakiongozwa na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi viongozi hao pia waliitaka serikali kusambaza vyakula vya msaada, dawa, mablanketi na vyandarua vya mbu kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.

“Vile vile, tunaikata serikali kutoa fedha kupitia Mamlaka ya Kusimamia Barabara za Mashambani (KeRRA) kwa ajili ya kukarabati barabara na madaraja ambayo yameharibiwa na mvua hii,’ akasema jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo bunge, Nairobi.

Aliandamana na wenzake, Ali Wario (Bura), Teddy Mwambire (Ganze), Mishi Mboko (Likoni), Ruweidha Obbo (Mbunge Mwakilishi, Lamu) na Mbunge wa Malindi Kaskazini Owen Baya.

Wabunge hao pia waliitaka Wizara ya Elimu kufanya ukaguzi katika shule zilizoathirika na mafuriko ili kuzifanyia ukarabati kabla muhula wa kwanza kuanzi Januari mwaka ujao.

‘Uharibifu ambao kufikia sasa umesababishwa na mafuriko umeshinda uwezo wa serikali za kaunti na Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF). Hii ndio maana tunaomba serikali ya kitaifa iingilie kati ili watu wetu wasiendelee kuathirika,’ akasema Bw Wario.