Habari Mseto

Wabunge wa Rift Valley waanza kutoka mafichoni


WABUNGE wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kutoka eneo la Bonde la Ufa wamejitokeza baada ya kujificha kwa wiki kadhaa wakihofia hasira za raia kutokana na hatua yao na kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2024 uliokataliwa na umma.

Wabunge wengi walirejea katika maeneobunge yao wikendi iliyopita wakijumuika na raia katika matanga, makanisa na shughuli nyingine za kijamii.

Hata hivyo, walikuwa waangalifu katika hotuba zao.

Wabunge hao waliwaomba msamaha wakazi wa maeneobunge yao kwa kufeli kuzingatia matakwa yao ya kuifanyia mageuzi Mswada huo uliochangia vijana kuandamana na hatimaye kuvamia majengo ya bunge mnamo Juni 25, 2024.

Wakitoa kumbukumbu kuhusu fujo za siku hiyo, wabunge hao walielezea jinsi walivyofurushwa na vijana hao walioteketeza sehemu ya majengo ya bunge, wakavunja fanicha na kuharibu stakabadhi muhimu.

Wabunge hao walisema hayo Jumamosi walipohudhuria mazishi ya aliyekuwa Katibu wa Wizara Joseah Sang katika eneo la Kapkatet, Kaunti ya Kericho.

Miongoni mwao ni kiongozi wa wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot, Johana Ng’eno (Emurua Dikirr), Hillary Koskei (Kipkelion Magharibi), Nelson Koech (Belgut), Kibet Komingoi (Bureti), Brighton Yegon (Konoin) na Mbunge Mwakilishi wa Kericho Beatrice Kemei.

Bi Kemei alipuuzilia mbali madai kuwa alizirai wakati wa purukushani hizo katika majengo ya bunge.

“Nimesikia watu wakisema kuwa nilizirai kwa mshtuko baada kutoroka kutoka bunge vijana wa Gen-Z walipoingia mle. Ningependa kusema kuwa hayo madai si kweli,” akasema.

Bw Ng’eno ambaye alizuru kaunti za Bomet, Kericho na Narok wiki moja kabla alitoa wito kwa raia kuwaruhusu wabunge wao wawatembelee na wawaombe msamaha kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2024.

Mbunge huyo alisema alilazimishwa na waandamanaji hao kutoa tai yake ili wamwachilie huru.

Ajibu kwa mzaha, Bi Kemei aliongeza hivi: “Kile ambacho Ng’eno hawaambii ni kwamba alitoa tai yake, koti na miwani na kujifanya kuwa mhudumu wa bunge ili kukwepa kushambuliwa.”

Akizungumzia sera za kiuchumi zinazoendeshwa na utawala wa Rais William Ruto, Bw Koech (Mbunge wa Belgut) alikubali kuwa ni nzuri lakini wananchi wanafaa kuhamasishwa vizuri kuzihusu.