Wabunge wa Wiper watishia kutema Kalonzo

Wabunge wa Wiper watishia kutema Kalonzo

Na CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge wa Wiper wametisha kumtelekeza kiongozi wao Kalonzo Musyoka ikiwa atakubali kuwa mgombea mwenza wa kiongozi wa ODM Raila Odinga au Naibu Rais William Ruto.

Wakiongozwa na Seneta wa Kitui Enock Wambua, wabunge hao wapatao sita hata hivyo walitangaza kuwa wataendelea kumuunga mkono Bw Musyoka ikiwa ataweka kando ndoto yake ya kuwa rais na kuunga mkono mmoja wa vinara wenza katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

“Ikiwa kiongozi wa chama chetu atafanya uamuzi wa kuunga mkono Raila Odinga katika kinyang’anyiro kijacho cha urais tunamhakikisha matokeo mawili. Kwamba atatembea safari hiyo pekee yake na pili jamii ya Wakamba pamoja na mamilioni ya wafuasi wake kote nchini katu hawatamsamehe,” Bw Wambua akasema Jumatano kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Huku akikariri kuwa OKA ingali imara, seneta huyo alishikilia kuwa hawataunga mkono Bw Odinga hata kama ataamua kujiunga na muungano huo changa.

Bw Wambua akafafanua kwamba “hii ni sauti ya wananchi kule mashinani”.

“Vinara wote wanne wa muungano huu wamehitimu kuwa Rais wa Kenya. Kwa hivyo, tungependa kusema hapa leo (jana Jumatano) kwamba hata Raila akijiunga na OKA, sharti aunge mkono mmoja wa vinara wetu; Kalonzo, Musalia Mudavadi, Moses Wetang’ula au Seneta Gideon Moi. Kwa hivyo, hatuna shida ikiwa kiongozi wetu ataamua kuunga mkono mmoja wa vinara hao wanne,” akasisitiza Bw Wambua.

Wengine walioandamana naye ni pamoja na wabunge; Makali Mulu (Kitui ya Kati), Daniel Maanzo (Makueni), Dan Mwashako (Wundanyi) na Mbunge Mwakilishi wa Kituo Irene Kasalu.

Awali, Bw Musyoka amewahi kusema kuwa atakuwa “mjinga” ikiwa atamuunga mkono tena Bw Odinga baada ya kufanya hivyo mara mbili katika chaguzi za 2013 na 2017.

Duru ziliambia “Taifa Leo” kwamba Bw Musyoka amekuwa akipata presha kutoka kwa kambi ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba akibali kuunga mkono Bw Odinga ambaye anaonekana kuungwa mkono na wandani wa kiongozi huyo wa taifa.

You can share this post!

Serikali yatangaza ukame kuwa janga

GWIJI WA WIKI: Dkt Deborah Nanyama Amukowa