Wabunge waachwa vinywa wazi kuambiwa Sh6.2 bilioni za zabuni haramu za Kemsa zitalipwa

Wabunge waachwa vinywa wazi kuambiwa Sh6.2 bilioni za zabuni haramu za Kemsa zitalipwa

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE walipigwa butwa baada ya Afisi ya Mkuu wa Sheria kuwafichulia kuwa serikali italipa Sh6.2 bilioni, pesa za mlipa ushuru, kwa zaidi ya kampuni 100 zilizopewa zabuni haramu za kuiuzia Mamlaka ya Dawa Nchini (KEMSA) bidhaa za kinga ya corona.

Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto Jumatano aliambia kamati ya bunge inayochunguza sakata hiyo kwamba hata katika hali ambapo zabuni zilipeanwa kinyume cha sheria, wawasilishaji bidhaa sharti walipwe.

“Kuhusiana na zabuni za kuwasilisha vifaa vya kujikinga corona (PPEs) tulithibitisha kuwa zilitolewa kinyume cha sheria. Lakini tayari mahakama zimetoa uamuzi katika suala hilo kwamba wafanyabiashara husika sharti walipwe kulingana na bei ya sasa ya bidhaa hizo sokoni,” Bw Ogeto akaambia Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC).

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Sheriff Nassir imekuwa imechunguza sakata hiyo ambapo usimamizi wa Kemsa ulipeana zabuni ya thamani ya Sh6.2 bilioni kinyume cha sheria, kati ya Machi na Aprili 2020.

Hata hivyo, alisema japo maafisa wa Kemsa waliohusika na utoaji zabuni hizo watashtakiwa kwa makosa, wafanyabiashara husika wataendelea kupambana mahakama ili walipwe.

Bw Ogeto alisema kila kesi itashughulikiwa kulingana na ushahidi na hali iliyopelekea kutolewa kwa kila zabuni.

“Sheria ni wazi kwamba hata katika hali ambapo sheria haikufuatwa mhusika mmoja hafai kufaidi na mwingine kupata hasara,” akasema.

Ogeto ambaye ni Afisa mwajibikaji katika Afisi ya Mkuu wa Sheria Kihara Kariuki, alisema japo ni haki kwa wafanyabiashara hao kulipwa, Kamati ya Muda inapasa kuundwa kujadiliwa na wakurugenzi wa kampuni hizo kuhusu suala hilo.

Kauli ya afisa huyo iliibua mjadala mkali miongoni mwa wanachama wa PIC wakiuliza ni kwa nini kampuni hizo zinapasa kulipwa hata baada ya asasi za uchunguzi kuthibitisha kuwa zabuni hizo zilitolewa kinyume cha sheria.

Wakipinga kutolewa kulipwa kwa kampuni hizo, wabunge Mishi Mboko (Likoni), Julius Melly (Tinderet), Tom Kajwang (Ruaraka) na Mbunge wa Budalang’I Raphael Wanjala walisema hatua hiyo ni sawa na kuhalalisha makosa kwa sababu zabuni hizo zilikuwa zimethibitishwa kuwa haramu.

“Hakuna mantiki kwa Afisi ya Mkuu wa Sheria kuruhusu malipo hayo baada ya kandarasi hizo kuthibitishwa kutolewa kinyume cha sheria,” akasema Bi Mboko.

Bw Wanjala alipendekeza kwamba KEMSA irejeshe bidhaa hizo corona (PPEs) kwa kampuni husika kwa maafisa wa mamlaka hiyo walikiuka sheria walipokuwa wakitoa zabuni hizo.

“Kwa kulipia bidhaa hizo zilizowasilishwa kwa Kemsa, serikali itakuwa inatakasa sakata chafu. Nini itazuia wakuu wa mashirika mengine ya serikali kutoa zabuni kinyume cha sheria kwa imani kuwa hatimaye zitalipiwa?” akauliza Wanjala.

Bw Nassir alisema kamati yake itatoa mapendekezo makali yatakayohimiza uzingatiwaji wa sheria kuwa kigezo kikuu cha ulipaji wa wawasilishaji bidhaa kwa asasi za serikali.

“Mapendekezo yetu yatakaza kamba na kuhimiza utiifu wa sheria katika utoaji zabuni katika mashirika ya serikali. Tumejitolea kuzima kutokea kwa sakata kama hii ya Kemsa katika shirika lingine la serikali,” akaeleza.

Miongoni mwa kampuni zilizopewa zabuni katika Kemsa kinyume cha sheria ni pamoja na Megascope healthcare Ltd (bidhaa za thamani ya Sh1.1 bilioni), Regal Freighters (Sh270 milloni), Northlink GSC Ltd (Sh135 milloni), Meraky Health Care (Sh140 milioni).

Zingine zilikuwa; Everywhere Distributors (Sh118 milioni), La Miguela Holding Ltd (Sh180 milioni), Shop ‘N’ Buy Ltd (Sh970milioni), Medlife Biological Ltd (Sh240milioni) na Komtel Kenya Ltd (Sh283m). Kwenye orodha hiyo pia kulikuwa kampuni za Wallabies Ventures (iliyopewa zabuni ya thamani ya Sh75m) na Crown Healthcare (Sh50 milioni).

Uchunguzi maalum ulioendeshwa na Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu Novemba mwaka jana, uligundua kuwa Sh2.3 bilioni zilipotea katika sakata ya utoaji zabuni katika Kemsa. Hii ni kwa sababu mamlaka hiyo iliuziwa bidhaa kwa bei ya juu kupita kiasi.

Bi Gathungu alielekeza kidole cha lawama kwa wakuu wa Kemsa kwa kukiuka sheria za utoaji zabuni za umma na hivyo kupelekea kupotea kwa fedha hizo za umma.

Ripoti ya uchunguzi huo pia ilibaini ulaghai ambapo kuliwa na njama, ya kufaidi kutokana na pesa za umma, kati ya maafisa wakuu wa Kemsa na wakurugenzi wa kampuni hizo zilizopewa zabuni ya thamani ya mabilioni ya fedha kinyume cha sheria.

Kulingana na Bi Gathungu, Kemsa ilinunua bidhaa nyingi kupita kiasi na ambazo zingali katika maghala ya asasi hiyo ya serikali.

Ikiwa bidhaa hizo (PPEs) zitauzwa kwa bei ya sasa, Kemsa itakomboa Sh4 bilioni pekee, na kupelekea hasa Sh2.3 bilioni.

Ripoti hiyo na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ilionyesha kuwa Kemsa ilielekeza fedha Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) katika mpango wa ununuzi wa PPEs bila kupata idhini kutoka kwa Wizara ya Afya.

You can share this post!

ICC yampata aliyekuwa kiongozi wa LRM na hatia

Wewe si ‘hasla’, ulikuwa karibu na Mzee Moi...