Habari MsetoSiasa

Wabunge wadai muungano mpya wa kisiasa watokota 2022

April 16th, 2019 2 min read

STANLEY KIMUGE na WYCLIFF KIPSANG

BAADHI ya viongozi wa Jubilee wameelezea uwezekano wa muungano wa kisiasa kati ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge Maoka Maore (Igembe Kaskazini), Peter Mwathi (Limuru) na mbunge maaalum Maina Kamanda waliungana na wenzao wa Kanu William Kamket (Tiaty) na Gladwell Cheruiyot (Baringo) kwenye hafla ya kuchangisha fedha katika kanisa la AIC Churo Girls katika eneobunge la Tiaty mnamo wikendi.

Bw Kamanda alisema aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Kanu kwa muda mrefu katika tawi la Nairobi, hivyo hana tatizo kushirikiana na chama hicho.

“Nimesema muunge mkono Kanu, kwani kuna baadhi ya watu waliokuwa wakidai kuwa ndio wanalidhibiti eneo hili kisiasa. Nataka kuwaambia kuwa kesho watakuwa wenye wafuasi wachache na Kanu itakuwa na wengi,” akasema Bw Kamanda.

Mbunge huyo alidai eneo la Kati limebadilisha mwelekeo wake wa kisiasa, ambapo sasa linaunga mkono ajenda ya umoja wa nchi inayoendelezwa na Rais Uhuru Kenyatta, Raila Odinga, Seneta Gideon Moi, kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Amani (ANC) Musalia Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya, Moses Wetang’ula.

“Ikiwa mtawaona baadhi ya wabunge kutoka Kati wakienda kinyume na msimamo huo, mfahamu kuwa wanajitafutia pesa. Wapiga kura wengi wanaunga mkono juhudi za Rais kuleta umoja nchini,” akasema Bw Kamanda katika matamshi yaliyoonekana kulilenga kundi la ‘Tanga Tanga’ ambalo linahusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Bi Cheruiyot alisema kuwa, kama wanachama wa Kanu, hawana shida yoyote ikiwa Bw Odinga ama Seneta Moi atakuwa rais.

“Mrengo wetu unaunga mkono handisheki kikamilifu. Kuna baadhi yetu wanaomuunga mkono Odinga, huku wengine wakimuunga Gideon. Tutazungumza na kushauriana,” akasema Bi Cheruiyot.

Kwa upande wake, Bw Maore alisema kuwa wanashirikiana na wenzao katika Kanu kwa kuwa ni “marafiki wao wa zamani.”

“Kuna tofauti kubwa kati yetu tuliyo katika Team Kenya na wengine (Team Tanga Tanga). Sisi ni marafiki wa Kanu na tumekuja hapa kuwaambia kwamba ufisadi ndilo suala kuu linalomsumbua Rais Kenyatta kwa sasa,” akasema Bw Maore.

Seneta Moi alikuwa ametarajiwa kuhudhuria hafla hiyo lakini akatuma mchango wake kupitia Bw Kamket.

Bw Kamanda alisema kwamba Rais Kenyatta alimteua kama mbunge maalum baada ya kunyang’anywa ushindi wake na baadhi ya watu katika JP.

“Ninajua kuwa nilishinda uchaguzi huo lakini nikanyang’anywa na baadhi ya watu walio chamani. Hata hivyo, rais alinionea imani kwa kunirejesha tena Bungeni,” akasema.

Ijumaa iliyopita, baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei na mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali walikitaka chama hicho kuwachukulia hatua viongozi wanaozua migawanyiko chamani.

Walisema kuwa lazima Bw Kamanda anyang’anywe wadhifa wake, kwani ni miongoni mwa watu wanaokigawanya chama.