Habari Mseto

Wabunge wafundisha wakazi mbinu za kukabili corona

March 25th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI mbalimbali wamejitokeza ili kuhamamisha umma kuhusu virusi vya corona.

Wabunge wanne kutoka Kisii na naibu gavana walitoa vifaa vya watu kuoshea mikono huku wakiwarai wazingatie usafi na masharti yaliyotangazwa na waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe.Wabunge hao Ben Momanyi (Borabu), Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba), Richard Tong’i (Nyaribari Chache), na Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini) waliandamana na Naibu Gavana Joash Maangi katika eneo la Kijauri.

Bw Momanyi alitoa ndoo na sabuni na dawa za kunawia mikono na kuagiza vyombo hivyo viwekwe katika masoko na stani zote za magari katika eneobunge lake.

Bw Richard Onyonka aliwasihi wamiliki wa nyumba za kupangisha watafakari kuhusu kuwapunguzia wapangaji kodi ya kila mwezi ya nyumba hizo.

“Wakenya wengi wameathirika katika shughuli zao pamoja na kukosa kuendesha biashara zao. Huenda wapangaji wengi wakawa na ugumu wa kulipa kodi,” akasema.

Bw Maangi naye aliwataka viongozi waweke kando tofauti zao za kisiasa na kushirikiana kikamilifu katika kuhamasisha umma.

“Huu si wakati wa kunyosheana vidole. Janga hili ni la ulimwengu mzima na sisi kama viongozi twafaa kuzika tofauti zetu katika kaburi la sahau na kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huu ambao umeleta hasara na maafa mengi,” akasema.

Katika Kaunti ya Nakuru, chama cha makahaba kinaitaka serikali ya kaunti hiyo izingatie jinsi ambavyo wafanyabiashara wake watakavyopata misaada ya chakula na pesa za kulipa kodi.

Chama hicho kinadai kuzorota kwa biashara wakati huu ambapo dunia inajizatiti kudhibiti janga la virusi vya corona.Tangu Jumatatu, wanachama walisema wamekuwa na ugumu wa kupata wateja hasa baada ya baa na maeneo mengine ya burudani kufungwa.

“Mara nyingi tulitegemea watalii katika baa za hapa mjini na kumbi za burudani lakini kwa sasa hali imegeuka na huduma kukwama. Tunaomba serikali iingilie kati tupate chakula na jinsi ya kulipa kodi,” akasema mwenyetiki wa chama hicho ambaye tumebana jina lake.

Barabara ya Kanu Street, mjini Nakuru inaongoza kwa idadi kubwa ya vilabu, huku takwimu zikionyesha eneo zima lina zaidi ya baa 200.

Wakati wa mahojiano, baa nyingi zilikuwa zimetiwa kufuli huku maafisa wa polisi wakiendelea kushika doria.

Kwingineko katika Kaunti ya Kisumu, mwanaume mmoja anataka serikali imlazimishe baba yake mdogo ajitenge na umma kwa siku 14.Lawrence Okoth anasema kaka (amu) mdogo wa babaye, Bw Domnick Owuor Oloo alitangamana na hata kusalimiana na padri wa Kanisa Katoliki aliyeongoza mazishi Siaya, kisha akathibitishwa kuugua virusi vya corona.

“Tunataka serikali imtenganishe babangu huyo aliyetangamana na padri huyo kwa karibu sana pamoja na wanakijiji waliohudhuria mazishi hayo mnamo Machi 14,” akasema.

Bw Okoth alisema alipata ujumbe kutoka kwa ukoo wake ulioko Ambira pamoja na marafiki waliomweleza kuwa, babaye mdogo alionekana akimsalimu padri na kukaa karibu naye wakati wa mazishi.

Ripoti za Wycliffe Nyaberi, Phyllis Musasia, Richard Maosi na Brenda Awuor