Habari MsetoSiasa

Wabunge 'waingizwa box' na Uhuru kuhusu malipo

September 19th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WABUNGE wamekubaliana na Rais Uhuru Kenyatta kwamba hawafai kujiongezea mishahara na marupurupu kiholela bila kuhusisha Tume ya Kutathmini Mishahara (SRC).

Kwa msingi huu, wabunge wameondoa vifungu katika mswada wa Tume ya Huduma ya Bunge (PSC) waliyoipatia mamlaka hayo ya kuwaongezea mishahara na marupurupu watakavyo.

Mnamo Jumatano, Kamati ya Bunge kuhusu Sheria (JLAC) ilifuta vifungu vya 30 na 43 vya mswada huo ambavyo walikuwa wamepatia PSC nguvu za kuwaongezea mishahara na marupurupu bila kushauriana na SRC.

Rais Kenyatta alikataa mapendekezo yao akisema hakuna nyongeza ya mishahara inayofaa kutekelezwa bila kuhusisha SRC.

Mwenyekiti wa JLAC, William Cheptumo, alisisitiza kuwa kufuta vifungu hivyo hakutapokonya PSC majukumu yake inayotwika na katiba.

Vifungu vilivyofutwa vilipatia PSC nguvu za kutekeleza majukumu mengine yanayostahili kukimu maslahi ya wabunge.

Kama mswada huo ungeidhinishwa, tume ingekuwa na uwezo wa kuongeza wafanyakazi wa bunge mishahara na marupurupu bila kuhusisha SRC.

PSC ingekuwa na nguvu za kuongeza wabunge mishahara baada ya kila miaka mitatu au wakati wowote ikihisi kuna haja ya kufanya hivyo.

Spika wa Bunge Justin Muturi ambaye ni mwenyekiti wa PSC alikuwa ametetea mapendekezo hayo akisema yalifaa kuhakikisha maslahi ya wabunge yamezingatiwa kikamilifu.

Bw Muturi alidai wabunge ni watumishi wa umma na hawafai kubaguliwa wakati wa kulipwa marupurupu.

Akikataa pendekezo hilo, Rais Kenyatta alisema kikatiba, ni SRC pekee iliyo na nguvu za kuweka viwango vya mishahara na akawataka wabunge kufanyia mswada huo mabadiliko.

Kwenye ripoti iliyowasilisha bungeni Jumatano, JLAC ilisema imefuta vifungu hivyo, ikisisitiza kuwa majukumu ya SRC yamefafanuliwa vyema kwenye katiba.

“Kamati inapendekeza kuwa wabunge wanafuta vifungu vyote vinavyokiuka katiba kutoka mswada huu,” alisema Bw Cheptumo kwenye ripoti aliyowasilisha bungeni.

Katika mswada huo, wabunge walitaka wawe wakiamua marupurupu wanayopaswa kulipwa wakizuru mataifa ya kigeni na maeneo mbali mbali nchini.

SRC ilienda kortini wabunge walipojipatia marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.

Aidha, wabunge wamekuwa wakitaka walipwe marupurupu ya kukodi chumba cha kulala wakiwa jijini Nairobi kuhudhuria vikao.

Kulingana na SRC, wabunge wanapaswa kulipwa mshahara wa Sh621,000, Sh8,000 marupurupu kwa wenyekiti wa kamati wakihudhuria vikao na wanakamati wanapaswa kulipwa Sh5,000 kwa kila kikao.

SRC pia imewapa bima ya matibabu, na mikopo ya gari na nyumba miongoni mwa marupurupu mengine.