Habari

Wabunge wainunia serikali wakijadili masaibu ya Yassin Juma

September 11th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Alhamisi waliishutumu Serikali kuwatelekeza Wakenya wanaokamatwa na kuteswa katika mataifa jirani huku wakilaani kukamatwa kwa mwanahabari Yassin Juma aliyetiwa mbaroni nchini Ethiopia Julai 2, 2020.

Viongozi hao kutoka mirengo ya Jubilee sasa wanaitaka Serikali kupitia Wizara ya Mashauri ya Kigeni kuishurutisha Ethiopia itaje sababu ya kukamatwa kwa Mkenya huyo na iombe msamaha.

Wakiongozwa na Mbunge wa Eldas Aden Keynan, wabunge hao walisema inasikitisha kuwa japo Kenya ni taifa kuu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati imeruhusu mataifa jirani kuidharau na kuichulia kuonekana nchi isiyo na nguvu.

“Mheshimiwa Spika, bunge hili haliwezi kutosheka na taarifa kutoka kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni kwamba mwanahabari Yassin Juma yuko huru ilhali haijatueleza kiini cha kukamatwa kwake. Tunataka teulezwe sababu ya kukamatwa kwa Mkenya huyo nchini Ethiopia na kudhulumiwa kwa zaidi ya siku 40 korokoroni jijini Addis Ababa,” akasema.

Bw Keyna pia alilaumu Shirika la Maendeleo kati ya Mataifa ya Ukanda huu (IGAD) na Umoja wa Afrika (AU) kwa kukaa kimya wakati ambapo majirani wa Kenya wanatesa raia wake.

Mbunge wa Sako Dido Rasso alisema familia ya Juma na Wakenya kwa ujumla hawawezi kusherehekea kuachiliwa kwake kabla ya Serikali ya Ethiopia kuwaambia makosa ambayo alifanya na kisha iombe msamaha.

“Haina maana kwetu kusherehekea kuachiliwa kwake bila kuambiwa makosa aliyofanya. Kisheria, ikiwa alishiriki uhalifu alipaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria namna ambavyo serikali Kenya pia inafaa kuwaadhibu wahalifu wa asili ya mataifa ya kigeni,” akasema.

Wabunge hao walikuwa wakitoa kauli zao kuhusiana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni kupitia mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Masuala ya Kigeni Katoo Ole Metito kuhusu kukamatwa kwa Bw Yassin.

Hii ni baada ya Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, mwezi jana, kuitaka Wizara hiyo kutoa taarifa kuhusu mwanahabari huyu baada ya kuripotiwa kuwa alikuwa ameambukizi Covid-19 akiwa korokoroni.

Bw Juma aliachiliwa mnamo Agosti 17, 2020 baada ya kupona corona. Awali mahakama moja iliamuru aachiliwe baada ya kutopatikana na kosa lolote.

Mkenya huyo alikamatwa pamoja na wanahabari wengine wa asili ya Ethiopia walipokuwa wakikusanya habari kuhusiana na machafuko yaliyotokea baada ya mauaji ya mwimbaji wa kabila la Oromo Hachalu Hundessa.

Hundessa, ambaye pia ni mwanaharakati wa kutetea haki za wanyonge, anajulikana kwa nyimbo zake zenye maudhui ya kisiasa, alipigwa risasi na akauawa jijini Addis Ababa. Kifo chake kilisababisha machafuko ya kikabila jijini humo.

Wakati wa fujo hizo, maafisa wa polisi waliwakamata wanahabari pamoja na wanachama wa makundi ya upinzani na kiongozi wao Jawar Mohammed.

Polisi walidai Bw Juma, na wanahabari wenzake, walikuwa washirika wa viongozi hao wa upinzani na kwamba wao ndio walichochea vita.

Walipelekwa kortini na kufunguliwa mashtaka ya kupanga kuwashambulia na kuwaua mafisa wa usalama wa Ethiopia.

Hata hivyo, mahakama aliamuru kuwa waachiliwe kwa dhamana baada ya maafisa wa polisi kufeli kutoa ushahidi wa kuwahusisha na uhalifu wowote.

Alhamisi, Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi alisema kukamatwa kwa mwanahabari huyo nchini Ethiopia na kuteswa kwake, pasina Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Ubalozi wa Kenya jijini Addis Ababa kuingilia kati, kunaonyesha kuwa Kenya haina nguvu za kidiplomasia.

“Kenya inapasa kudhihirisha kuwa ina nguvu za kidiplomasia kutetea masilahi ya raia wake katika nchi za kigeni.

“Mataifa mengine hufanya kila yawezayo kufuatilia haki za raia wao wanapokamatwa katika nchi za kigeni kuonyesha kuwa wanawajali. Tunapasa kuambiwa waziwazi sababu iliyopelekea Juma kutupwa gerezani kinyume cha sheria,” akasema Bw Wandayi.

Nao wabunge Leisamis MP Malimo Marselino (Leisamis), Julius Melly (Tinderet) Haika Munebe (Mbunge Mwakilishi wa Taita Taveta) na mbunge wa Suna Magharibi Peter Masara waliitaka Serikali ya Ethiopia kumlipa fidia Bw Juma.

Bw Masara alisema Wakenya wengi wamekuwa wahangaishwa na maafisa wa usalama wa Uganda katika Kisiwa cha Migingo lakini serikali haijafanya lolote kukomesha mwenendo huo.

“Madhila ya Juma yaliangaziwa zaidi katika vyombo vya habari kwa sababu ni mwanahabari. Swali langu ni je, nani atawatetea Wakenya wengine wanaozuiliwa kinyume cha sheria katika mataifa ya Uganda, Tanzani na Sudan Kusini?” akauliza.