WABUNGE waisuta TSC kwa kubebesha walimu mzigo wa mafunzo ya ziada

WABUNGE waisuta TSC kwa kubebesha walimu mzigo wa mafunzo ya ziada

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne jioni walipinga vikali mpango wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) ya kuwataka walimu kulipa Sh6,000 kila mwaka kugharamia mafunzo yao ya ziada.

Wakiunga mkono ombi kutoka kwa walimu wa Nairobi lililosomwa kwa niaba yao bungeni na Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba wabunge waliisuta TSC kwa kufanya uamuzi huo bila kuwahusisha walimu.

Wabunge walisema wazo hilo ni bora lakini mafunzo hayo yanapaswa kugharamiwa na TSC wala sio walimu ambayo walisema wanapokea mishahara finyu na hivyo hawawezi kumudu gharama ya mafunzo hayo.

“Ni jambo la kawaida kwa asasi yoyote ile kuwahitaji wafanyakazi wake kupokea mafunzi ya ziada. Lakini asasi husika ndio inapaswa kugharamia mafunzo hayo sio wafanyakazi. Kwa hivyo, TSC ambayo ndio mwanajiri wa walimu inapaswa kubeba mzigo huo kwa niaba ya wanafunzi watakaofaida wali sio walimu,” akasema mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga.

Naye Mbunge wa Nyando Jared Okello alisema walimu hawapati mishahara mikubwa na hivyo hawafai kubebeshwa mzigo mwingine wa kulipia mafunzo yao ya ziada.

“Kuwahitaji walimua kulipa Sh6000 kwa kila somo katika mafunzo hayo ni kuwanyanyasa walimu hao. Kwa hivyo, naliomba Bunge hili kusitisha mpango huu hadi mipango mwafaka itakayowekwa kutekeleza mpango huu,” akasema mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha ODM.

Naye Mbunge Maalum David Sankok alihoji vigezo ambavyo TSC iliumia kuteua vyuo vikuu vinne ambavyo vitatoa mafunzo hayo. Mbili kati ya vyuo hivyo, Chuo Kikuu cha Riara na kile cha Mount Kenya, ni vyuo vya kibinafsi.

“TSC ni tume ya kikatiba na ambayo inafadhiliwa na fedha za umma. Mbona ipeane zabuni kama hii kwa vyuo vikuu vya kibinafsi bila kuelezea vigezo ilivyotumia?”, Bw Sankok akauliza.

Kauli yake iliungwa mkono na wabunge, John Mbadi (Suba Kusini), Martha Wangare (Gilgil) na Mbunge Maalum Wilson Sossion.

Katika ombi lau kwa bunge walimu hao wa Nairobi ambao ni wanachama wa chama cha kutetea masilahi ya walimu wa shule za upili (KUPPET) walilitaka bunge kuiamuru TSC iitishe mkutano wa wadau kabla ya kutekeleza mpango huo.

“Utekelezaji wa mpango huu wa mafunzo ya ziada kwa walimu usitishwe kwa muda hao wadau wote watakapoitwa kwa kukubaliana kuhusu namna ya kuyaendesha,” akasema Bw Milemba, ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa wa Kuppet.

Chini ya mpango huo walimu watahitajika kupata mafunzi katika nyanja sita (module), kila moja ikichukua kipindi cha miaka mitano. Kwa hivyo, watahitajika kulipa jumla ya Sh180,000 kukamilisha mafunzo hayo.

You can share this post!

Uteuzi wa Chiloba ni njama ya kuboronga uchaguzi 2022...

Hatimaye Bomet yauza majanichai Iran