Habari Mseto

Wabunge waitaka NCPB iwaondolee wakulima masharti

January 31st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sita kutoka eneo la North Rift jana walitaka Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuondoa masharti magumu iliyowawekea wakulima wa mahindi kabla ya kununua mahindi yao, wakiyataja masharti hayo kama dhalimu.

Wakiongozwa na Mbunge wa Soy Caleb Kositany, viongozi hao waliitaka bodi hiyo kuanza kupokea mahindi kutoka kwa wakulima “bila masharti magumu” kulingana na agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

“Ni zaidi ya wiki tatu baada ya Rais Kenyatta kuamuru NCPB kuanza kununua mahindi kutoka kwa wakulima lakini inasikitisha kuwa shughuli hiyo imecheleweshwa huku wakulima wakiwekewa masharti yasiyo na maana na dhalimu. Tunaitaka bodi hii kufungua depo zake mara moja na kuanza kununua mahindi ili wakulima wapate pesa za kujiandaa kwa msimu huu wa upanzi,” akasema kwenye kikao na wahabari katika majengo ya bunge.

Alikuwa ameandamana na wenzake; Kangogo Bowen (Marakwet Mashariki), William Kisang’ (Marakwet Magharibi), Dkt Robert Pukose (Endebess) na Mbunge Maalum Sammy Saroney.

Bw Kositany alisema haina maana NCPB kuwahitaji wakulima kuwasilisha hati-miliki za mashamba yao, vitambulisho vya kitaifa, nambari ya utambulisho kutoka Mamlaka ya Ushuru (KRA) na hati ya ukodishaji kabla ya mahindi yao kununuliwa.

“Wakulima wengi kutoka eneo la North Rift hawana hati-miliki za mashamba. Kwa hivyo, tunaaamini kuwa sharti kama hili linalenga kuhujumu lengo la serikali la kuimarisha uzalishaji wa chakula ambalo ni mojawapo ya Ajenda Nne Kuu,” akasema Bw Kisang.

Wabunge hao pia waliutaka usimamizi wa NCPB kuondoa sharti kwamba wakulima ambao watawasilisha zaidi ya magunia 400 sharti wapate idhini kutoka kwa Bodi ya Kusimamia Shirika la Uhifadhi wa Chakula Nchini (SFROB).

Wakati huo huo, wabunge watatu kutoka uliokuwa mkoa wa magharibi wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili wakulima miwa waweze kulipwa.

Mbw Emmanuel Wangwe (Navakholo, Jubilee), Dan Wanyama (Webuye Mashariki, Jubilee) na Justus Murunga (Matungu, ANC) pia waliitaka serikali kutoa malipo hayo (Sh2.6 bilioni) kabla ya bajeti ya muda kuwasilishwa bungeni hapo Aprili mwaka huu.

“Wakulima wa miwa kutoka magharibi mwa Kenya wanaendelea kuteseka kwani hawajalipwa mpaka sasa licha ya ahadi zilizotolewa na mawaziri Henry Rotich (Fedha) na Mwangi Kiunjuri (Kilimo). Tunamtaka Rais kuingilia kati suala hili ili Sh2.6 bilioni za wakulima zitolewe,” akasema Bw Wangwe.

Mbunge huyo ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo alidai kuwa watoto wa wakulima wa miwa hawajaripoti shuleni kwa sababu ya serikali kuchelewesha pesa hizo.

“Watoto wa wakulima wa miwa pia wana haki ya kwenda shuleni sawa na watoto wa wakulima wa mazao mengine kama kahawa na chai ambao tayari wamelipwa. Pesa za CDF hazitoshi kwani sheria inaturuhusu kutumia Sh10 milioni pekee,” akasema.

Naye Bw Wanyama pia alimtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuingilia kati suala hilo kwa “sababu yeye pia anatoka eneo kunakokuzwa miwa kwa wingi.”