Habari Mseto

Wabunge waitaka serikali ikomeshe mauaji Samburu

September 17th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Samburu wameitaka serikali kuimarisha usalama katika eneo bunge la Samburu Kaskazini ili kukomesha visa vya mauaji ya raia na wizi wa mifugo.

Hii ni kufuatia kisa ambapo mama mmoja mjane aliuawa kwa kupigwa risasi na wahalifu usiku wa kuamkia Jumatano katika kijiji cha Masikita, eneo la Baragoi.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge jana, Mbunge wa Samburu Kaskazini Alois Lentoimaga na mwenzake wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda walimtaka Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuamrisha operesheni ya kuwasaka wakora hao katika eneo la Baragoi.

“Tumechoka na visa vya mauaji ya raia wasio na hatia na wizi wa mifugo kila mara katika eneo hili la Baragoi. Tumtaka Bw Matiang’i na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai waamuru operesheni kali ya kusaka na kuwakamata wakora hawa ambao wamevuruga maisha katika eneo hili,” akasema Bw Lentoimaga.

Alisema marehemu kwa jina Mama Tiwani Persila, 45, alimiminiwa risasi tano kifuani mwendo wa saa moja jioni Jumanne alipotoka nje ya nyumba baada ya kusikia kilele zikipigwa.

“Inakera kuwa watoto wawili wa mjane huyo sasa wamebaki bila mlezi kufuatia kuawa kwa mama yao. Tumeambiwa kuwa wahalifu hao walitorokea bonde la Suguta baada ya kutekeleza mauaji hayo,” Bw Lentoimaga akaeleza.

Naye Bi Lesuuda alimtaka Bw Mutyambai kuwahamisha maafisa wa polisi walioko Baragoi akisema wameshindwa na kazi.

“Ikiwa polisi wanawaogopa wahalifu hawa nani atawasaidia wananchi wasio na silaha? Inspekta Jenerali wa Polisi awaondoe hawa na kuleta kikosi ambacho kinaweza kupambana na wakora hawa,” akasema Bi Lesuuda.

Alitisha kuandaa maandamano makubwa katika eneo hilo kulaani mauaji ya raia katika eneo hilo ikiwa hatua zozote hazitachukuliwa kudhibiti hali ya utovu wa usalama katika eneo hilo.

Wabunge hao walitaka serikali kuwarejeshea bunduki askari wa akiba ambao walipokonywa silaha hizo katika operesheni iliyoendesha na serikali mwaka jana.

Bw Lentoimaga na Bw Lesuuda walisema bunduki ambazo hutumiwa kutekeleza uhalifu katika eneo hilo huingizwa nchini kutoka mataifa jirani ya Sudan Kusini na Ethiopia.

“Hali hii vile vile husababishwa na hatua ya serikali kufeli kukomboa bunduki ambazo hutwaliwa na wahalifu hao baada ya wao kuwashambulia maafisa wa usalama. Kwa mfano, tunaamini kuwa baadhi ya bunduki hizo ni zile ambazo zilipokonywa maafisa 41 waliouawa katika bonde la Suguta mnamo 2012,” akasema Bw Lentoimaga.

Eneo hilo hushuhudiwa visa vya mauaji na wizi wa mifugo kila mara huku baadhi ya wanasiasa wakiekezewa kidole cha lawama.

Kwa mfano, mwezi jana Seneta wa Samburu Steve Lelengwe alikamatwa na kuandikisha taarifa katika kituo cha Maralal kwa tuhuma za kuchochea visa vya utovu wa usalama.

Na mwaka jana, Bw Lentoimaga alihojiwa na maafisa wa upelelezi wa jinai (DCI) mjini humo kwa tuhuma za kuchochea mapigano na wizi wa mifugo katika eneo bunge lake la Samburu Kaskazini.