Habari MsetoSiasa

Wabunge waitaka serikali kuwalipa wazee wa vijiji

March 27th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI itaanza kuwalipa wazee wa mitaa marupurupu kutokana na huduma wanazotoa kwa ushirikiano na machifu na manaibu wao.

Hii ni endapo serikali itatekeleza hoja iliyopitishwa Jumatano bungeni.

Kulingana na hoja hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Tharaka, George Murugara, serikali inafaa kuwalipa wazee hao kama ishara ya kutambua mchango wao katika kuboresha utawala mashinani.

Bw Murugara alisema kazi za wazee hao ni pamoja na udhibiti wa usalama kupitia mpango wa ‘Nyumba Kumi’, utatuzi wa aina mbalimbali ya mizozo, ufafanuzi wa sera za maendeleo za serikali kuu na ushirikishaji wa shughuli za utoaji vitambulisho.

“Kwa hivyo, kupitia hoja hii Bunge linaitaka serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Masuala ya Usalama kubuni sera za kuongoza uajiri na ulipaji marupurupu kwa wazee hawa,” akasema.

Akiunga mkono hoja hiyo, Mbunge wa Malava, Malulu Injendi, alisema Serikali ya Kitaifa inafaa kuiga mfano wa serikali za kaunti ambazo huajiri na kuwalipa wasimamizi hadi katika ngazi ya vijijini kusimamia utekelezaji wa miradi.

Mbunge maalum David Sankok (pichani juu) alisema wazee hao huchangia sana kusuluhisha kesi nyingi katika ngazi za kifamilia na kiukoo.

Wabunge wengine waliounga mkono hoja hiyo ni Eric Machangi (Runyenjes), Martin Owino (Ndhiwa), Robert Pukose (Endebess) na Alfred Agoi (Sabatia).

“Hawa wazee wanafaa kulipwa kwa sababu nyakati zingine wao huhatarisha maisha yao wakihudumia wananchi kwa niaba ya serikali kuu,” akasema Bw Machangi.

Mnamo 2016 Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani Karanja Kibicho alitangaza kuwa serikali ingetenga Sh1.2 bilioni za kuwalipa wazee wanaoshiriki shughuli za kupambana utovu wa usalama vijiji.

Hata hivyo, serikali haijaweza kutekeleza ahadi hiyo.

Awali, mnamo 2014 jaribio la aliyekuwa Seneta wa Pokot Magharibi John Lonyangapuo (sasa Gavana) la kuandaa mswada wa kuilazimu serikali kuwalipa wazee wa mitaa mishahara liligonga mwamba baada ya kukosa kuungwa mkono na baadhi ya maseneta.