Na Faith Nyamai
WANAOHITIMU kutoka vyuo vikuu wataendelea kulipa mikopo yao kwa riba ya asilimia nne baada ya wabunge kukataa pendekezo la kupunguzwa kwa riba hiyo hadi asilimia tatu.
Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu pia wamekataa pendekezo la kuongezwa kwa muda wa kulipa mikopo hiyo kutoka mwaka mmoja hadi miaka mitano.
Kwenye ripoti iliyowasilishwa bungeni wiki jana, kamati hiyo ilisema kuwa mapendekezo hayo yaliyoko kwenye mswada wa marekebisho ya sheria ya bodi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu (HELB) yataiathiri kifedha.
Bodi hiyo ambayo pia hutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kadri, huwatoza faini ya Sh5,000 kila mwezi, wale wanaofeli kulipa mikopo yao.
“Kamati hii inaamua kuwa pendekezo la kupunguza riba hadi asilimia tatu kila mwaka litaathiri uwezo wa Helb kugharimia elimu ya wanafunzi wa vyuo vikuu,” ikasema kamati hiyo inaoyoongozwa na Mwakilishi wa Kike wa Busia, Bi Florence Mutua.
Mswada huo uliodhaminiwa na Mbunge Maalum Gideon Keter pia unapendekeza kuondolewa kwa riba kwenye mikopo ambayo Helb hutoa kwa watu wenye ulemavu.
Pia unapendekeza kuwa faini ya Sh5,000 kila mwezi itozwe wanaofeli kulipa mikopo baada ya wao kupata ajira au miaka mitano baada ya wao kuhitimu.
Kulingana na Bw Keter, wahitimu huchukua zaidi ya miaka mitano kabla ya kupata ajira na hivyo sio sawa kwa Helb kuwatoza faini hiyo kubwa kwa kuchelewa kulipa mikopo.
Katika ripoti yake Kamati hiyo ya Bunge inasema kuwa riba ya asilimia nne inayotozwa na Helb kwa mikopo ni ya chini kuliko kiwango cha mfumko wa bei nchini wa kima cha asilimia 5 kwa wastani ndani ya miaka mitatu iliyopita.
“Kwa hivyo, thamani halisi ya kiasi cha mkopo kilichotolewam hupunguza baada ya muda kwa sababu kiwango cha riba huwa ni chini ya kiwango cha kupanda kwa gharama,” ikasema ripoti hiyo.
Wabunge pia walisema kuwa kuwa kupunguza kiwango cha riba, mswada huo unaipokonya Helb mamlaka yake katika usimamizi wa mikopo.
Wabunge pia walisema Helb hutegemea pesa inazopata kutoka kwa wahitimu wanaolipa mikopo ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi wengine.
“Kwa mfano katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 bodi hiyo ilikusanya jumla ya Sh4.5 bilioni kutoka kwa wanafunzi wa zamani. Pesa hizi ndizo hutumika kuunda hazina ya kitaifa itakayotumika kutoa mikopo kwa vizazi vijavyo,” ripoti hiyo ikasema.