Habari Mseto

Wabunge wakataa ushuru kwa pensheni

June 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameondoa pendekezo kwenye Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2020 lililohitaji kutoza ushuru malipo ya uzeeni ambayo wazee waliostaafu hupokea kila mwezi.

Kwenye ripoti walioiwasilisha katika Bunge la Taifa mnamo Alhamisi jioni, wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha walisema ushuru huo utawaathiri vibaya wazee hao ilhali hawana mbinu mbadala za kujitafutia mapato.

“Kutozwa ushuru kwa malipo ya pensheni ya wazee waliostaafu kutawaumiza zaidi hasa wakati huu ambapo uchumi umeathirika kutokana na makali ya virusi vya corona. Huu ndio wakati ambapo serikali inapaswa kuwalinda watu hawa badala ya kuwanyanyasa,” ikasema ripoti hiyo iliyotiwa saini na wanachama wote wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao Joseph Limo.

Waliwahakikishia wazee hao kwamba hawataruhusu malipo yao yapunguzwe hata kwa senti moja. Kulingana na taratibu za kisheria, hatima ya wazee sasa itabaki mikononi mwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ndiye ataamua kama atakubaliana na wabunge, au atakataa uamuzi wao.

Kulingana na mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani mnamo Aprili, serikali ilipendekezo kutoza ushuru wa mapato kwa malipo ya pensheni ya wazee wenye umri wa miaka 65 kwenda juu.

Viwango vya ushuru huo vilipangiwa kufafanuliwa kwenye kanuni za utekelezaji wa pendekezo hilo ambazo zitatolewa na Wizara ya Fedha kwa ushirikiano na Mamlaka ya Malipo ya Kustaafu (RBA).

Mswada huo pia ulipendekeza kwamba mapato yanayotokana na Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) yatozwe ushuru endapo utapitishwa na kuwa sheria. Lakini, kwenye ripoti yake, Kamati ya Bunge kuhusu Fedha pia imebatilisha pendekezo hilo.

Mapendekezo hayo yalikuwa yameibua malalamishi mengi kutoka kwa wazee, wataalamu wa masuala ya uchumi pamoja na maafisa wa NSSF wakisema yanaenda kinyume na sera ya serikali ya kulinda maslahi ya wakongwe.

Serikali inakumbwa na hali ngumu kujitafutia hela za kuendesha shughuli za kitaifa, kwani kiasi kikubwa cha fedha kinafaa kutumiwa kulipa madeni ya takriban Sh6.2 trilioni ambayo yamechukuliwa na Kenya kufikia sasa.

Hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na janga la corona pia imechangia taabu zaidi kwa juhudi za serikali kujaza hazina yake ya fedha kwa kiwango kinachofaa.