Wabunge wakataa vipengele kwenye mswada wa fedha vinavyoongeza gharama ya maisha

Wabunge wakataa vipengele kwenye mswada wa fedha vinavyoongeza gharama ya maisha

NA CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Fedha imepinga mapendekezo ya Wizara ya Fedha ambayo yangechangia kuongezeka zaidi kwa bei za bidhaa za kimsingi na hivyo kupandisha gharama ya maisha.

Kwenye ripoti kuhusu Mswada wa Fedha 2022 iliyowasilishwa bungeni mnamo Jumanne, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Homa Bay Gladys Wanga, imepinga pendekezo la kutozwa ushuru wa thamani ya ziada (VAT) kwa unga wa mahindi na ngano.

Katika bajeti aliyowasilisha bungeni mnamo Aprili 7, 2022 Waziri wa Fedha Ukur Yatani alipendekeza kuwa bidhaa hizo zitajumuishwa miongoni mwa zile ambazo hutozwa ushuru huo wa kima cha asilimia 16, serikali ikilenga kukusanya Sh53.4 bilioni zaidi.

Hiyo ingechangia kupanda zaidi kwa bei ya bidhaa hizo ambayo tayari ziko juu. Kwa mfano, bei ya unga wa mahindi wa mahindi umepanda kutoka Sh100, kwa paketi ya kilo mbili mnamo Januari hadi Sh150 wakati huu, kwenye maduka Nairobi.

Nayo bei ya unga wa ngano imepanda kutoka Sh130 Januari hadi Sh170 kwa paketi moja ya kilo mbili wakati huu.

Kamati hiyo pia ilikataa pendekezo la Wizara ya Fedha la kuongeza ushuru unaotozwa washiriki wa michezo ya kamari na pombe.

Kamati hiyo inahofia kwamba huenda ongezeko la ushuru unaotozwa pombe ukachangia waraibu kugeukia pombe haramu na ya bei ya chini, yenye madhara kwa maisha yao.

“Aidha ongezeko la ushuru unaotozwa kampuni za kamari na washiriki wa michezo ya bahati nasibu huenda likachangia waraibu wa mchezo huo kuhamia kampuni za kigeni. Hatua hii itaathiri uchumi wa nchi kwani serikali haitaweza kukusanya fedha inazotarajia,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa na Bi Wanga.

Kamati hiyo pia ilipinga pendekezo la Wizara ya Fedha kutoza gharama ya matangazo ya michezo ya kamari na pombe, ikisema “pendekezo hilo halifai”.

Wabunge wanachama wa kamati hiyo pia walipinga nyongeza ya ushuru unaotozwa pikipiki za bodaboda zinazonunuliwa kutoka nje, kutoka Sh12,185.16 hadi Sh13,403.64 kila moja,

“Ongezeko la ushuru unaotozwa bodaboda halifai kwa sababu litaathiri zaidi ya vijana 2.4 milioni wanaotegemea sekta hiyo kama chanzo cha mapato,” ripoti hiyo ikasema.

Kamati hiyo pia imeondoa sehemu katika Mswada wa Fedha unaopendekeza chupa za glasi zilizotengenezwa nchini zitozwe ushuru wa kima cha asilimia 25. Hii ni afueni kwa watengenezaji sharubati (juisi) na pombe.

  • Tags

You can share this post!

Ubinafsi watajwa kiini cha viongozi kuhama kila mara

MAPISHI KIKWETU: Kuku na supu ya uyoga

T L