Habari MsetoSiasa

Wabunge walimeza hongo ndani ya choo, Wamuchomba afichua

August 15th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Kiambu Gathoni Wamuchomba amedai kuwa baadhi ya wabunge wenzake walimtusi alipokataa kupokea hongo iliyokuwa ikitolewa bungeni, ili kuwafanya wabunge kuitupilia ripoti iliyobaini kulikuwa na sukari hatari nchini.

Akizungumza katika mtaa wa mabanda wa Kiandutu, Thika mnamo Jumanne wakati wa kutoa msaada wa vyakula kwa kituo cha kuwarekebisha watoto wa mitaani, Bi Wamuchomba alisema pesa zilizotolewa zilikuwa ‘zimelaaniwa’ na kuwa hangekula hongo na kuhatarisha maisha ya Wakenya.

Mbunge huyo alisema baadhi ya wabunge walipokea rushwa hiyo kwenye vyoo vya bunge, akisema waliokataa kupokea waliitwa waoga.

“Hizo ni pesa ambazo zinaweza kusababisha laana zisizoepukika, siwezi kuzipokea. Nataka kumweleza spika kuwa nataka kuhusishwa kwenye uchunguzi kwa kuwa nilikuwa bungeni wakati pesa hizo zilikuwa zikitolewa.

Niliona walipoenda kuzipokea n ahata wengine walitutusi kwa kukosa kuungana nao,” akasema Bi Wamuchomba.