Habari MsetoSiasa

Wabunge walivyoimba nyimbo za kusifu Nyayo bungeni

February 12th, 2020 1 min read

Na Charles Wasonga

WABUNGE mnamo Jumatatu alasiri walivunja sheria za bunge na kuimba nyimbo za kumsifu Rais Mstaafu marehemu Daniel arap Moi bungeni wakati wa kikao maalam cha kumuombeleza kiongozi huyo.

Wakiongozwa na Mbunge wa Ijara Sophia Abdi Noor, wabunge hao waliimba nyimbo ‘Tawala Kenya Tawala, ‘Ooh Kanu Yajenga Nchi’ na ‘Fimbo ya Nyayo” kwa takriban dakiki 10 Spika Justin Muturi akitizama huku akitabasamu.

Nyimbo hizo zilikuwa maarufu zaidi wakati wa utawala wa Mzee Moi uliodumu kwa miaka 24.

Katika rambirambi zao, wabunge hao walimtaja rais huyo wa zamani kama kiongozi mzalendo aliyechangia amani na utulivu sio tu nchini bali katika mataifa kadhaa ya Afrika.

Kiongozi wa wengi Aden Duale alisema miradi mingi ambayo Mzee Moi alianzisha wakati wa utawala wake ndiyo iliyoweka msingi wa maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi hasusan elimu.

“Moi alianzisha shule nyingi wakati wa utawala wake na hivyo kuwawezesha watoto wetu kupata nafasi ya kusoma katika pembe zote za nchi hii,” akasema.

Moi aliongoza chini ya kauli mbiu “siasa mbaya maisha mbaya” ambayo ni funzo kwetu viongozi wa sasa ambao tunaendesha siasa ambazo haziwafaidi watu wetu,” akaongeza Mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Mbunge wa Suba Kaskazii Millie Odhiambo Mabona alisema Moi aliomba msamaha kwa wale ambao aliwakosea.

Bw Otiende Amolo (Rarieda) alisema hatua ya Moi kuomba msamaha kwa wale ambao huenda aliwakosea ni ishara kwamba alikuwa kiongozi mwenye hekima nyingi.

“Kwa hivyo, wakosoaji wake waache roho yake ipumzike kwa amani,” akaeleza.Naye Mbunge wa Soy Caleb Kositany alimtaja marehemu Moi kama kiongozi mvumilivu na mpenda amani.

“Kwa mfano, licha ya kurushiwa matusi na wananchi alipokuwa akimpokeza Mwai Kibaki uongozi mnamo 2002, hakujali,” akasema Mbunge huyo wa Jubilee.

Baadhi ya wabunge wenye umri mdogo walimsifu Moi kutokana na mpango wake wa kutoa maziwa kwa wanafunzi wa shule za msingi.