Habari MsetoSiasa

Wabunge wamkabili Matiang'i kwa kupokonywa walinzi

April 28th, 2019 1 min read

Na SAMWEL OWINO

WAZIRI wa Usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i Ijumaa alikuwa na wakati mgumu kueleza wabunge sababu ya serikali kuwapokonya walinzi baadhi ya wenzao wanaomuunga Naibu Rais William Ruto.

Kwenye mkutano na viongozi wa bunge mjini Mombasa, wabunge walimshinikiza Dkt Matiang’i kuwaeleza aliyeamuru Katibu wa wizara hiyo Karanja Kibicho kuondoa walinzi wa baadhi ya wenzao.

Joto katika mkutano huo lilianza kupanda wakati wabunge walipomzomea kiongozi wa wachache John Mbadi ambaye aliwataka wabunge walioathiriwa wasilalamike kwa sababu hata wabunge wa upinzani wamewahi kujipata katika hali sawa na hiyo na hawakulalamika.

“Tulijipata katika hali hiyo na hatukupiga kelele. Sasa ni zamu yenu,” Bw Mbadi alisema huku akipigiwa kelele na wabunge hasa wanaomuunga Dkt Ruto.

Spika Justin Muturi hata hivyo aliepuka suala hilo na kuzungumzia majukumu ya bunge na seneti.

Kabla ya wanahabari kuagizwa kuondoka mkutanoni, Dkt Matiang’i aliepuka suala hilo na kuzungumzia Ajenda Nne kuu za serikali na jinsi mabunge yote mawili yanaweza kushirikiana kusaidia serikali.

Waliohudhuria kikao cha faragha waliambia Taifa Jumapili kwamba joto lilipanda wabunge wakimlaumu waziri kwa kuingia shughuli za bunge kwa kuadhibu wale wanaotofautiana na serikali.