Wabunge wamtaka Rais apunguze gharama

Wabunge wamtaka Rais apunguze gharama

WABUNGE wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio wamempongeza Rais William Ruto kwa kupunguza bei ya mbolea lakini wakamtaka kutekeleza mipango mingine ya kuimarisha uzalishaji wa chakula.

Wakichangia katika mjadala kuhusu hotuba ambayo Rais alitoa bungeni mnamo Alhamisi wiki jana, wabunge hao walimtaka kupunguza bei ya mbegu, miongoni mwa pembejeo nyingine za kilimo. Hotuba hiyo itajadiliwa kwa vikao vinne.

“Rais anastahili pongezi kwa kupunguza bei ya mbolea hadi Sh3,500 kutoka Sh6,000. Rais sasa anapaswa kupunguza bei ya mbegu, dizeli inayotumika kwa wingi na wakulima, kemikali za kuangamiza wadudu waharibifu miongoni mwa mahitaji mengine,” akasema Mbunge wa Imenti Kaskazini, Bw Rahimu Dawood.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tharaka Gitonga Murugara aliitaka serikali kusambaza chakula cha msaada kwa wakazi wa eneo bunge lake na kaunti ya Tharaka Nithi kwa ujumla.

“Hotuba ya Rais ilikuwa nzuri kwa sababu iliangazia masuala yenye umuhimu mkubwa kwa raia wa kawaida kama vile mikakati ya kupunguza gharama ya maisha. Lakini wakati kama huu watu wetu wanahitaji chakula na maji kwa dharura zaidi,” akasema.

Nao wabunge wa Azimio James Nyikal (Seme-ODM), Peter Salasya (Mumias Mashariki-DAP-K) na Julius Sunkuli (Kilgoris, Kanu) walisifu hotuba ya Rais Ruto lakini wakamtaka kuelekeza pesa nyingine katika sekta ya kilimo.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Maoni ya umma kuhusu GMOs yanafaa...

Chipukizi hodari wa chesi apania kuvunja rekodi mashindano...

T L