Habari MsetoSiasa

Wabunge wanawake wanaomtetea Jumwa wamepotoka – Gladys Wanga

March 5th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi Mwanamke wa Homa Bay Gladys Wanga, Jumanne alitofautiana na wabunge wanachama wa Muungano wa Wabunge Wanawake (KEWOPA) ambao walitangaza kuwa watamuunga mkono Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa aliyefurushwa kutoka ODM.

Bi Wanga alisema wabunge hao wanawake wakiongozwa na Mbunge wa Kandara Esther Wahome walikuwa wakitoa madai ya uwongo kwa kuisuta ODM kwa kumfurusha Bi Jumwa kwa utovu wa nidhamu. Vil vile, Bi Jumwa anatuhumiwa kuunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto ya kuwania urais 2022.

“Mimi ni mwanachama wa KEWOPA na hatujaketi, kujadili na kufikia uamuzi kuhusu suala hili. Pili, suala la kufurushwa kwa Bi Jumwa ni la ODM na halihusu Kewopa. Kwa hivyo, inashangaza kuwa wenzangu wanakutana na kudai kuwa muungano wetu, KEWOPA, unatetea mwenzetu Jumwa,” akasema Bw Wanga.

“Mwenzetu alishauriwa aombe msamaha lakini akadinda. Lakini Bw Suleiman Dori ambaye aliomba msahama amepewa muda wa siku 60 kabla ya kesi yake kusikizwa upya na kuamuliwa,” Bw Wanga akaambia Taifa Leo.

Mbunge huyo Mwakilishi wa Homa Bay ambaye ni mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo, alisema hayo saa chache baada ya kundi la wabunge 10 wanawake kuhutubia wanahabari wakiapa kusimama na Bi Jumwa.

Walisema kufurushwa kwa Mbunge huyo wa Malindi kunaashiria kuwa ODM haiheshimu misingi ya kidemokrasi na katiba inayotoa nafasi kwa Wakenya kutangamana bila kujali miegemeo yao ya kisiasa.

“Sisi kama KEWOPA tutapinga huu mpango wa ODM kumfukuza mwenzetu Aisha katika ngazi zote za mahakama hadi Mahakama ya Juu. Kwa hivyo, tunamtaka Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu kutoondoa jina la Jumwa kutoka orodha ya wanachama wa ODM. Na Spika Muturi asichukue hatua yoyote dhidi ya mwenzetu kwa kutangaza kiti chake kuwa wazi,” akasema Bi Wahome.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wabunge wa mrengo wa Jubilee pekee. Bi Getrude Mbeyu (Mbunge Mwakilishi wa Kilifi) ndiye alikuwa mbunge wa kipekee wa ODM aliungana na wenzake tisa kumtetea Bi Jumwa.

Mbunge mwakilishi wa Isiolo Rehema Jaldesa alidai kuwa kufurushwa kwa Bi Jumwa kunalenga kuhakikisha kuwa bunge halitimizi hitaji la kikatiba kwamba jinsia moja haifai kuwakilishwa na zaidi ya thuluthi mbili bungeni.