Habari Mseto

Wabunge wanne kufika kwa DCI kuhusu video ya ngono

February 24th, 2019 2 min read

Na KIPCHUMBA SOME

WABUNGE wanne wameitwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuandikisha taarifa kuhusiana na video feki ya ponografia iliyobadilishwa kumpaka tope Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Wajir, Bi Fatuma Gedi.

Wabunge Aden Keynan (Eldas), Abdihakim Osman Mohamed (Fafi), Rehema Dida Jaldesa (mwakilishi wa wanawake Isiolo) na Purity Wangui Kuria Ngirici (mwakilishi wa wanawake, Kirinyaga) wanapaswa kufika katika ofisi za DCI kesho na Jumanne.

“Idara ya DCI inachunguza madai ya kuharibia mtu jina kupitia faili iliyofunguliwa katika kitengo cha kukabiliana na uhalifu sugu ambapo walioorodhesha wametajwa,” afisa anayechunguza kesi hiyo, Wiso J.M. alisema kwenye barua aliyomwandikia karani wa bunge Michael Sialai mnamo Februari 21.

“Tafadhali waeleze kwamba wafike katika makao makuu ya DCI, kwenye barabara ya Kiambu saa nne kusaidia katika uchunguzi,” inasema barua ya Bw Wiso.

Bw Keynan na Bw Mohamed wanatarajiwa kufika mbele ya wapelelezi Jumatatu nao Bi Jaldesa na Bi Ngirici wanatarajiwa kufika Jumanne.

Hata hivyo, haifahamiki iwapo watafika kama alivyoomba mchunguzi wa kesi baada ya afisa wa masuala ya sheria wa bunge, Kuyioni Josphat, kumshauri Bw Sialai kwamba DCI inafaa kuwasiliana na wabunge hao moja kwa moja badala ya kuwaita kupitia karani wa bunge.

“Kesi inayochunguzwa haitokani na utendakazi wa majukumu ya wabunge. Na kwa hivyo, tunapendekeza kwamba DCI iwasiliane moja kwa moja na wabunge husika,” aliandika.

Video inayodaiwa kumuonyesha Bi Gedi akiwa katika hali tatanishi na mwanamume asiyejulikana ilipakiwa mtandaoni Desemba mwaka jana na inashukiwa ilitolewa kwenye tovuti za ponografia na kukarabatiwa kuonyesha uso wa mbunge huyo.

Bi Gedi alisema sio yeye aliyekuwa kwenye video hiyo na akaitaja kama kazi ya mahasimu wake wa kisiasa katika bunge la Kaunti ya Wajir.

Polisi tayari wamewakamata watu sita kuhusiana na video hiyo feki, wawili kutoka tovuti ya Tuko ambayo ilikuwa ya kwanza kuchapisha video hiyo na washukiwa wanne kutoka serikali ya Kaunti ya Wajir. Inasemekana mmoja wa washukiwa hao alilipwa Sh2 milioni kuunda na kusambaza video hiyo.

Bi Gedi na Bw Keynan wamekuwa wakipingana katika siasa za Wajir. Bw Keynan anamuunga Gavana wa sasa Mohamed Abdi Mohamud, naye Bi Gedi ni mfuasi wa aliyekuwa gavana Ahmed Abdullahi.

Bw Mohamud na Abdullahi wamekuwa wakizozana kufuatia matokeo ya uchaguzi wa ugavana wa 2018.