Makala

Wabunge waombwa kukataa kupitisha ushuru mpya kwa mapato ya wakulima

January 18th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa vyama vya wakulima wa mazao mbalimbali nchini wamewataka wabunge kupinga aina mpya ya ushuru wa mapato ambao serikali inapania kuwatoza wakulima.

Wanasema ushuru huo unaojulikana kama ‘Withholding Tax’ wa asimilia tano ya mapato ya wakulima utawaumiza wakulima zaidi ikizingatiwa kuwa wanakabiliwa na mzigo wa kulipa ada nyinginezo.

“Nawaomba wabunge wetu watupilie mbali kabisa pendekezo hili la kuwawekea wakulima mzigo mwingine kwa kuwatoza ushuru wa asilimia tano kwa mapato yao. Hili ni pendekezo ambalo limeletwa na Benki ya Dunia (WB) baada ya serikali kuanzisha mpango wa kutoa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima,” Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Wakulima Nchini (KFA) Kipkorir Arap Menjo akaambia Taifa Leo Jumatano kwa njia ya simu.

Kulingana na Bw Menjo, ushuru huo utarudisha nyuma ukuaji katika sekta ya kilimo na mikakati wa uzalishaji chakula toshelezi.

“Sekta ya Kilimo huchangia asilimia 22 ya Utajiri wa Nchini (GDP) na hutoa nafasi nyingi za ajira kwa watu wetu haswa wale wanaoishi mashambani. Lakini sisi kama wakulima sasa tuna hofu kwamba kupanda kwa gharama ya uzalishaji kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta na mzigo wa ushuru kutafifisha manufaa haya,” akaongeza.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Muungano wa Mashirika ya Kutetea Masilahi ya Wakulima wa Miwa Nchini (KNAFSO) Saulo Busolo alipinga ushuru huo mpya akiutaja kama “sumu kwa wakulima”.

“Pendekezo hilo ambalo liko kwenye Taarifa kuhusu Bajeti (BPS) ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 linafaa kukataliwa na wabunge na Wakenya kwa ujumla. Ushuru huo utaangusha kabisa sekta ya kilimo ambayo imekuwa nguzo ya uchumi wa nchini. Serikali inastahili kupunguza ushuru katika sekta hii badala ya kuongeza kwani hatua hiyo itadumaza uzalishaji,” akasema.

“Tofauti na miaka ya nyuma, Katiba sasa imewapa wabunge usemi mkubwa katika mchakato wa utayarishaji bajeti. Hii ndiyo maana nawataka wabunge kukataa ushuru huu wa ‘Withholding tax”,” akaongeza Bw Busolo ambaye ni mbunge wa zamani wa Webuye (sasa limegawanywa kuwa Webuye Mashariki na Webuye Magharibi).

Wiki jana, Mbunge Mwakilishi wa Nyeri Rahab Mukami pia alipinga kuanzishwa kwa ushuru huo wa kima cha asilimia tano kwa mapato ya wakulima wanaowasilisha mazao yao kwa vyama vya ushirika na makundi mengine yaliyosajiliwa na serikali.

“Hatutakubali wakulima wa kahawa kutozwa ushuru wa asilimia tano,” akasema.

Mbunge huyo alisema tayari wakulima hao wanazongwa na gharama kubwa ya uzalishaji na kuwaongezea ushuru zaidi itakuwa sawa na kuwanyanyasa.

Kulingana na taarifa ya BPS ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 iliyochapishwa na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u mnamo Desemba 18, 2023, serikali itapendekeza kuanzisha ushuru wa asilimia tano ya thamani ya mazao wanayowasilisha kwa vyama vya ushirika na makundi mengine.

Hii ina maana kuwa kila ikiwa pendekezo hilo litapitishwa kila mkulima atakuwa akilipa Sh5 kwa kila 100 kutokana na mauzo ya mazao yake.

Pesa hizo zitakatwa kabla ya mkulima kulipwa na kuwasilishwa kwa Idara ya Ushuru wa Mapato (Income Tax Dept) katika Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA).

Kulingana na Waziri Ndung’u, sekta ya kilimo nio mojawapa ya zile ambazo hazijakuwa zikitozwa ushuru ipasavyo ‘ilhali ina utajiri mkubwa na inaongoza katika uzalishaji’.

“Imekuwa vigumu kwa serikali kukusanya ushuru kutoka sekta ya Kilimo sawa na sekta ya kamari na biashara ya mtandaoni. Hii ndio maana serikali inapendekeza ushuru huu ili kuongezea mapato yake,” waziri akasema.

Pendekezo hilo litajadili litajadiliwa na wabunge kuanzia Februari 13, 2024, watakaporejea kutoka likizo ndefu.