HabariSiasa

Wabunge waongezewe mishahara, Wakenya wamewageuza benki – Atwoli

May 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SIKU chache baada ya juhudi zake za kutaka serikali iwape wafanyakazi nyongeza ya mishahara ya asilimia 15 kugonga mwamba, Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli sasa anaunga mkono nyongeza ya mishahara ya wabunge.

Akihutubia wanahabari Jumatatu jijini Nairobi, Bw Atwoli alisema mishahara ya wabunge inapasa kuongezwa ili kuwawezesha kutosheleza matakwa ya wananchi ambao huwaomba pesa kila mara.

“Huu mtindo wa wananchi kuwaomba wabunge pesa kila mara umepelekea baadhi ya viongozi hao kujihusisha katika ufisadi. Hii ndio maana ninaunga mkono, ninaonelelea kuwa wana kila haki ya kuongezewa mishahara,” Bw Atwoli akasema.

Kulingana na kinara huyo wa COTU, tabia ya Wakenya ya kuwaomba wabunge pesa kila mara ndiyo imechochea ufisadi nchini akisema; “hatuwezi kupambana na ufisadi wakati ambapo wale wanaoongozwa wanaendeleza tabia ya kuwaomba viongozi wao fedha kila mara,”

“Mkinichagua kisha mtarajie pesa kila mara kutoka kwangu, basi hiyo itamaanisha kuwa sharti nilipwe mshahara wa juu kama mbunge wenu,” akasema Bw Atwoli.

Akaongeza: “Ikiwa leo Mbunge anakuja katika eneobunge lako kuhudhuria mazishi na akatoa mchango wa Sh3,000 au Sh5,000 utawasikia watu wakilalamika kana kwamba ni lazima kwa mbunge huyo kutoa mchango mazishini. Watanung’unika kwa sababu wao hutarajia wabunge kutoa michango mikubwa; kuanzia Sh30,000 kwenda juu.”

Kianara huyo wa COTU alisema kuna baadhi ya wabunge ambao hutumia kati ya Sh300,000 na Sh600,000 kila wiki wanapotembelea maeneobunge yao; pesa ambazo wanatarajiwa kutoa kutoka kwa mishahara yao.

“Tumewageuza wabunge wetu kuwa mipango ya malipo ya uzeeni, tumewageuza mashirika ya akiba na mikopo (Sacco), tumewageuza wabunge wetu kuwa benki, tumewageuza wabunge wetu kuwa watu wa kutulipia karo na kila kitu…” Bw Atwoli akaongeza.

Kiongozi huyo wa Cotu alitoa wito kwa Wakenya kushiriki katika shughuli za kuwaletea mapato kama vile kilimo badala ya kutegemea viongozi wao kwa mahitaji yao ya kila siku.

“Hapa nchini, Mungu ametupa hali nzuri ya anga, tunaweza kufanya mambo mengi ya kutuletea mapato. Tunaweza kwenda shambani kuzalisha viazi kisha kuuza sokoni na kupata pesa kidogo… badala ya kugeuza wabunge wetu kuwa bima ya matibabu,” Bw Atwoli akasema.

Kauli ya Atwoli inajiri baada ya kutoa kwa habari kwamba wabunge na maseneta juzi walijitengea Sh936 milioni kama marupurupu ya nyumba iliyopendekezwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) 2018.

Hii ina maana kuwa kando na mishahara yao, wabunge na maseneta (ambao idadi yao ni 416) watapokea Sh250,000 kwa mwezi kila mmoja kama marupurupu ya nyumba. Hii ni licha ya pingamizi iliyotolewa na Hazina ya Kitaifa na Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC).

Iliripotiwa kuwa kila mbunge na seneta alipokea Sh2.25 milioni mwishoni mwa Aprili kwa sababu marupurupu hayo ya nyumba yalianza kulipwa Agosti mwaka 2018 wakati ambapo PSC iliidhinisha bajeti yake.