Habari MsetoSiasa

Wabunge wapagawa kwa siasa za 2022

March 11th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa mirengo ya Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga kwa upande mmoja, dhidi ya wenzao wa Naibu Rais William Ruto, Jumatano waliendelea kupagawa kwenye ushindani kuhusu uchaguzi wa urais 2022.

Wabunge wa mrengo wa Dkt Ruto waliwajibu wenzao wa handisheki wakimtaja Bw Odinga kama anayetumia urafiki wake na Rais Kenyatta kuvuruga serikali ya Jubilee na kuzamisha Naibu Rais kisiasa.

Wabunge hao wa handisheki walikuwa awali wamemtaka Dkt Ruto ajiuzulu.

Wakiwajibu wenzao, wanaowaunga mkono Bw Odinga na Rais Kenyatta, wabunge hao zaidi ya 50 walisema kuwa kiongozi Bw Odinga analenga kuigawanya Jubilee kisiasa, ili kujifaidi yeye mwenyewe.

Walisema kuwa ni mbinu ambayo amekuwa akitumia tangu jaribio la mapinduzi mnamo 1982.

“Raila ameteka mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa kutumia mikutano yake kumtusi Dkt Ruto. Kwa kujificha nyuma ya Rais Kenyatta, amesambaratisha maono ya Rais ili kujijenga kisiasa. BBI sasa imegeuka kuwa jukwaa la Odinga kuendeleza njama zake dhidi ya Dkt Ruto,” akasema Seneta wa Meru Mithika Linturi, ambaye ndiye alisoma taarifa hiyo kwa niaba ya viongozi hao.

Viongozi hao walimtetea vikali Dkt Ruto, wakisema kuwa ndiye kiongozi wa pekee ambaye amesimamisha mipango yake ili kuhakikisha kuwa Rais Kenyatta ametimiza malengo yake kisiasa.

Hivyo, walisema kuwa wale wanamkosoa Dkt Ruto kwa madai ya kutomheshimu Rais Kenyatta ni wanafiki.

“Raila anasahau kwamba amemwelekeza Rais Kenyatta kila aina ya matusi. Kinaya ni kwamba hajawahi kukana matamshi hayo, hata baada ya handisheki,” akasema Bw Linturi.

Walisema kuwa wanafahamu uwepo wa mipango ya kumwondoa Dkt Ruto uongozini, ili kumwezesha Bw Odinga kupata nafasi serikalini kama Msimamizi Mkuu wa Mawaziri.

Vita vya maneno vinaonekana kuendelea kushika kasi kati ya washirika wa viongozi hao wawili, wakionekana kuwa washindani wakuu kwenye uchaguzi wa urais mnamo 2022.