Habari MsetoSiasa

Wabunge wapendekeza Seneti iondolewe kwa katiba

February 19th, 2019 1 min read

NA FRANCIS MUREITHI

WABUNGE wawili kutoka Kaunti ya Nakuru wameapa kuwaongoza wananchi waliowachagua kufutilia mbali uwepo Bunge la Seneti kwenye katiba kufuatia matamshi ya maseneta wiki iliyopita kwamba bunge hilo linafaa kupewa hadhi kuliko lile ya Bunge la Kitaifa.

Samuel Arama wa Nakuru Magharibi na mwenzake wa Bahati, Kimani Ngujiri wamesema kwamba maseneta wamekuwa wakilala kazini na kukosa kumakinikia kazi yao ya kufuatilia namna fedha za kaunti zinavyotumika.

“Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kila mara imeonyesha jinsi ubadhirifu wa fedha umejikita katika kaunti mbalimbali, lakini maseneta hawajafanya chochote kuhakikisha fedha hizo hazitumiwi vibaya,” akasema Bw Arama.

Aliongeza kuwa Bunge la Seneti limekosa dira na sasa limeamua kutafuta visingizio ili kufunika kutowajibika kwake ndipo lionekana kama linalofanya kazi.

Bw Ngujiri naye aliwashtumu maseneta kwa kuandaa makongamano aliyosema si umuhimu na yanaharibu pesa za umma badala ya kufanya kazi ya kutafuta wawekezaji wa kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kaunti zao.

“Kama wabunge tuna mpango wa kila miaka mitano tunaotumia kujua utendakazi wetu kwa wananchi waliotuchagua. Bunge la Seneti halijawahi kutoa mpango wanaotumia kulinda matumizi mabaya ya fedha za umma katika kaunti wanazowakilisha,” akasema Bw Ngunjiri.

Wawili hao hata hivyo walitaja kushangazwa kwao na mtindo wa maisha wa baadhi ya maseneta ambao walisema wamekuwa matajiri kwa kipindi kifupi na wanamiliki majumba ya kifahari katika baadhi ya miji mikubwa nchini.