Habari MsetoSiasa

Wabunge wapinga kampeni kuunganisha jamii ya Abaluhya

April 11th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu kutoka Magharibi mwa Kenya wamepinga kampeni za kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula za kuunganisha jamii ya Waluhya wakiwataka kujiunga na chama cha Jubilee.

Wakiongea na wahabari Jumanne katika majengo ya bunge, Nairobi watatu hao, John Waluke (Pichani, Sirisia), Fred Kapondi (Mlima Elgon) na Janet Nangabo (Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Trans Nzoia) walisema hatua ya wawili hao ni ya kujitakia makuu baada ya “kudidimia kwa nyota yao ya kisiasa ndani ya NASA.”

“Jamii ya Waluhya tayari iko ndani ya serikali ya chama tawala cha Jubilee na hatutakubali itadanganye tena kwa kuhimizwa kujiunga na chama kipya kitakapobuniwa kupitia muungano wa Ford Kenya na ANC.

Sio haki kwa watu wawili kuhawadaa kugura serikali hii ambayo imetupa nafasi ya Spika wa Seneti, Kiranja wa Wengi, Mawaziri watu, Makatibu wa Wizara watatu na Naibu mkuu wa watumishi wa umma.

Mudavadi na Wetang’ula wajiunge na serikali badala ya kuwapotosha watu wetu,” akasema Bw Waluke

Mbunge huyo, ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usalama, alisema Mbw Mudavadi na Wetang’ula wameanzisha “injili” kuunganisha jamii ya Waluhya sio kutokana na sababu za maendeleo bali kwa sababu waliachwa nje katika mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

“Mbona hii kampeni imeanzishwa baada ya wawili hao kuhisi kutengwa katika ushirikiano wa Rais na Odinga. Mbona inajiri baada ya Wetang’ula kuondolewa katika wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti?,” akauliza Bw Waluke.

Naye Bw Kapondi alisema kampeni za Mudavadi na Wetang’ula inalenga kuwatenga watu wa jamii ya Sabaot na Teso ambao pia wanatoka eneo la hilo ambalo zamani lilijulikana na Mkoa wa Magharibi.

“Huu muungano unaonekana kama njama ya kuzitenga jamii za Wasabaot na Wateso ambazo zina mamilioni ya watu na asili yao ni ya mkoa wa magharibi.

Itakuwa bora kama Mudavadi na Wetang’ula watajiunga na Jubilee ili kuhubiri umoja badala hiii njama yao ya kuwagawanya watu wa eneo la magharibi kwa misingi ya kikabila, “ akasema Bw Kapondi ambaye ni mbunge wa chama cha Jubilee.

Bi Nangabo aliuliza ni kwa nini Mudavadi na Wetang’ula walishindwa kuwaunganisha Waluhya hapo awali waliposhikilia nyadhifa za uwaziri serikali.