Habari Mseto

Wabunge wapinga wakulima kupigwa msasa kabla ya kulipwa

August 23rd, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu kutoka eneo la North Rift wamepinga agizo la serikali kwamba wakulima waliwasilisha mahindi kwa mabohari ya Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) msimu uliopita wapigwe msasa kabla ya kupokea malipo yao.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano Mbw Alfred Keter (Nandi Hills, Jubilee), Silas Tiren (Moiben, Jubilee) na Ferdinand Wanyonyi (Kwanza, Ford Kenya) walidai kuwa hatua hiyo inalenga kunyanyasa wakulima hata zaidi.

“Wakulima wamesubiri wakisubiri kulipwa kwa muda wa miezi minane sasa na kunashangaa ni kwa nini serikali inataka wakulima wakaguliwe kwanza kabla ya kulipwa ilhali walipitia mchakato huo kabla ya kuwasilisha mahindi yao kwa NCPB,” akasema Bw Keter.

Mbunge huyo mbishani alisema serikali ina mbinu na mikakati ya kuwatambua wakulima bandia ambao huenda wakadai malipo ilhali hawakuwasilisha mahindi na haifai “kuwasumbua wakulima tena ikitaka wapigwe msasa”

“Serikali inafahamu wakora ambao wamekuwa wakijitokea kudai malipo. Inafaa kuwaandama wakora hao badala ya kuwasumbua wakulima ambao wamesubiri tangu mwaka jana kabla ya kulipwa,” akasema Bw Keter.

Naye Bw Tiren alimtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati suala hilo ili kuwaondolea usumbufu wakulima wa mahindi ambao wanangojea kulipwa kwa mahindi yao tangu mwaka jana.

“Serikali imetoa pesa ili wakulima walipwe. Sasa mbona tena waambiwe kuwa wanafaa kukaguliwa. Sielewi zoezi hili ni la nini. Naomba Rais aingilie suala hilo ili wakulima wetu walipwe haraka iwezekanavyo,” akasema Mbunge huyo.

Wiki jana, serikali ilitoa Sh1.4 bilioni kwa ajili ya kuwalipa zaidi ya wakulima 600 ambao waliwasilisha mahindi yao kwa depo za NCPB mwaka jana lakini mpaka sasa hawajalipwa.

Pesa hizo ni sehemu ya Sh3.5 bilioni ambazo wakulima hao kutoka kaunti za Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia na Nakuru wanadai serikali tangu mwaka jana.

Mapema mwaka huu, kulifichuliwa sakata ambapo zaidi ya Sh1.9 bilioni ambazo zilinuiwa kulipwa wakulima hao zililipwa wafanya biashara walaghai waliowasilisha mahindi katika NCPB wakidai hao ni wakulima.

Sakata hiyo inachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Kamati maalum iliyoundwa na Seneti.

Wiki hii serikali iliwataka walikulima ambao wanapania kufaidi kutokana na malipo hayo kuwasilisha nakala za vitambulisho vyao vya kitaifa, nambari za siri za KRA, picha ndogo, tiketi za upimaji uzani na maelezo ya benki kabla ya kulipwa pesa zao.

Wakulima pia wamepinga sharti hilo na kutaka liondolewe la sivyo wafanye maandamano katika miji mikuu katika eneo zima la North Rift.