Wabunge warejelea vikao huku wakitarajiwa kushughulikia miswada yenye umuhimu kitaifa

Wabunge warejelea vikao huku wakitarajiwa kushughulikia miswada yenye umuhimu kitaifa

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa linarejelea vikao vyake Jumanne, Novemba 9, 2021, baada ya likizo fupi ya majuma mawili ambapo wabunge walipata fursa ya kutembelea maeneo bunge yao kufahamu changamoto za wananchi.

Baadhi ya miswada ambayo imeorodheshwa kujadiliwa na Mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru wa bidhaa za mafuta,2021, Mswada kuhusu Ufadhili wa Kampeni za uchaguzi na Mswada wa marekebisho ya Katiba unaolenga kumpa Rais mamlaka ya kumfuta kazi Naibu wake.

Miswada hiyo mitatu itasomwa kwa mara ya kwanza katika kikao cha kuanzia saa nane na nusu alasiri kabla ya kuwasilishwa na Kamati husika za bunge kuanda vikao vya kushirikisha maoni ya umma kuhusu mapendekezo ya miswada hiyo. Baaada ya hapo miswada hiyo itarejeshwa bunge kujadiliwa kwa kina.

Mswada wa Mafuta unalenga kupunguza bei ya mafuta kwa kupunguza au kuondoa aina mbalimbali za ushuru unaotozwa bidhaa hiyo. Ushuru hizo ikiwemo ushuru wa ziada ya thamani (VAT) wa Sh8 kwa kila lita ya mafuta. Mswada huo unadhaminiwa na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha Gladys Wanga.

Ushuru wa juu unaotozwa bidhaa za mafuta ndio uliopelekea bei ya mafuta kupanda kupita kiasi kikubwa zaidi mwezi wa Septemba mwaka huu na kuibua malalamishi makubwa kutoka wa Wakenya, wanasiasa na watengenezaji bidhaa.

Kwa mfano bei ya mafuta aina petrol ilipanda hadi Sh134.7 kwa lita moja jijini Nairobi huku dizeli ikipanda hadi Sh115.5 kwa lita na mafuta taa ikipanda hadi Sh110.7.

Wabunge pia wanatarajiwa kuifanyia marekebisho Mswada kuhusu Ufadhili wa Kampeni ili kuondoa viwango vya fedha ambazo wanapaswa kutumia katika kampeni za kusaka uungwaji mkono kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.

Mswada wa marekebisho ya Katiba unaopendekeza kuwa Rais awe na uwezo wa kumfuta kazi Naibu Rais umedhaminiwa na Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni. Bw Kioni ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Marekebisho ya Katiba (CIOC).

Mswada huu umeibua pingamizi kubwa kutoka kwa wafuasi wa Naibu Rais William Ruto ambao wameahidi kuuangusha.

You can share this post!

Majaji watano wa mahakama ya juu waamuru Kananu aapishwe...

Chama cha madaktari nchini chapinga usimamizi wa KDF KEMSA

T L