Habari Mseto

Wabunge wasutwa kwa kupunguza bajeti ya SRC

June 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameshutumiwa vikali kwa kupunguza mgao wa fedha ambazo Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu (SRC) ilitengewa katika bajeti iliyowasilishwa bungeni wiki jana.

Kwenye malalamishi yaliowasilishwa bungeni Alhamisi, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Sera na Mizozo (ICPC) Ndungu Wainaina anasema kuwa hatua hiyo ni sasa na kuingilia mamlaka ya Wakenya na ukuu wa Katiba.

Bw Wanaina pia alitaja hatua hiyo ya wabunge kama matumizi mabaya ya afisi zao na mamlaka yao kama wabunge kwa kukiuka Katiba kuendeleza masilahi yao.

“Hii ni kielelezo cha bunge kukiuka sheria. Nchini Kenya katiba ndio kuu wala sio bunge. Hatua ya wabunge kupunguza mgao wa fedha kwa tume ya SRC ni kinyume cha Katiba,” Bw Wainaina akasema kwenye taarifa yenye malalamishi yake.

Mnamo Jumatano, Bunge la Kitaifa lilipunguza Sh95 milioni kutoka kwa Sh545,360, 000 zilizotengewa SRC kwenye bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich bungeni mnamo Alhamisi wiki jana.

Pendekezo hilo liliwasilishwa na Mbunge wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro na kuungwa mkono na wenzake; Wilberforce Oundo (Funyula) na David Sankok (Mbunge Maalumu).

Hatua hiyo ambayo huenda ikakwamisha shughuli za SRC ilijiri wakati ambapo wabunge waliidhinisha Sh1.8 trilioni zilizotengewa Serikali ya Kitaifa kwa ajili ya maendeleo na matumizi ya kila mara katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 unaoanza Julai 1, 2019.

Awali, tume hiyo inayoongozwa na Bi Lyn Mengich, ilitengewa Sh645,360,000 katika mwaka ujao wa kifedha lakini wiki jana wabunge wakapunguza mgao huo kwa kuondoa Sh125.6 milioni wakati walipitisha bajeti ya pili ya ziada.

Matumizi bila idhini

Hii ni baada ya kubainika kuwa SRC ilitumia Sh125.6 milioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2018/2019 bila idhini ya bunge.

Kati ya fedha hizo, tume hiyo ilitumia Sh99.17 milioni kununua magari na vifaa vingine, Sh20.4 milioni kukarabati afisi na Sh2.85 milioni kwa safari za humu nchini na matumizi mingineyo madogo.

Matumizi mengine yalikuwa Sh2 milioni za kugharamia operesheni za kawaida na Sh1.3 milioni kununua fanicha.

Jaribio la SRC la kutaka wabunge waliidhinishe matumizi ya pesa hizo liligonga mwamba.

Ingawa tume hiyo ilitaja kipengee cha 223 cha katiba kutetea hatua yao ya kutumia fedha hizo wabunge waliwapuuzilia mbali.

Kulingana na kipengee hicho, serikali, na asasi zake, zinaweza kutumia pesa ambazo hazijatengewa, kugharamia shughuli za dharura kama vile ukame, mafuriko na utovu wa usalama, lakini sharti ziombe idhini ya bunge ndani ya kipindi cha miezi miwili baada ya kutumia fedha hizo.

Wabunge walisema shughuli ambazo SRC ilitumia pesa hizo hazikuwa za dharura na kwamba tume hiyo ilifaa kusubiri idhini yao kabla ya kuzitumia.

“Haileweki ni kwa nini makamishna wa SRC walinunua magari mapya ilhali tume hiyo ina magari ambayo yalikuwa yakitumiwa na makamishna wa zamani. Pili, SRC sio tume mpya ambayo inahitaji kutumia pesa kukarabati afisi,” akauliza Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti, wiki jana.

SRC inavutana na wabunge kufuatia hatua yake ya kupinga marupurupu ya nyumba ya kima cha Sh250,000 kila mwezi ambayo walilipwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC).

Mwishoni mwa Aprili kila mbunge alipokea malimbikizi ya Sh2.1 milioni kila mmoja baada ya PSC kurejesha nyuma muda wa malipo ya marupurupu hao kuanzia Oktoa 5, 2018.

Huu ndio wakati ambapo Jaji wa Mahakama Kuu Chache Mwita alitoa uamuzi kwamba maafisa wote wa serikali wanafaa kulipwa marupurupu ya nyumba na serikali.

Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na Muungano wa Manaibu Gavana (Deputy Governor Forum) ulisema kuwa maafisa hao pia wanapasa kulipwa marupurupu ya nyumba.

Wabunge wamewekwa katika tapo la maafisa wa serikali (State Officers) kwa mujibu wa kipendee cha 260 cha Katiba lakini hawajakuwa wakipwa marupurupu ya nyumba.