Habari Mseto

Wabunge wataka ‘Kazi Mtaani’ isimamishwe

August 28th, 2020 1 min read

Na SAMWEL OWINO

WABUNGE sasa wanataka mradi wa serikali, ‘Kazi Mtaani’ usimamishe wakidai unatumika kama mwanya wa kupora fedha za umma.

Mradi huo ulizinduliwa mnamo Mei kama njia ya kuhakikisha vijana wanajikimu wakati ambapo virusi vya corona vilianza kuripotiwa nchini na kuathiri mapato yao.

Wabunge walimweleza Waziri wa Fedha Ukur Yattani kwamba mpango huo hauna maana wakisema serikali inafaa kuweka mikakati mipya ya kuhakikisha Kazi Mitaani inafanikiwa.

Mbunge wa Limuru Peter Mwathi alidai kuwa mradi huo unasababisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa vijana huku wengi wao wakifungiwa nje na baadhi kupendelewa kiasi cha kulipwa mara mbili.

“Serikali inafaa isitishe mpango huo na kuuratibisha vizuri kwa sababu vijana wote hawanufaiki na baadhi wameanza kuzozana tangu uanzishwe,” akasema Bw Mwathi.

Naibu Spika Moses Cheboi naye alisema serikali inahitaji kuhakikisha kwamba vijana wanalipwa vizuri kutokana na kazi za sulubu wanazozifanya.

“Ukienda kwenye maeneobunge yetu vijana hujishughulisha tu na kusafisha mabomba ya majitaka kila siku. Tutapiga hatua sana iwapo vijana hawa watafundishwa kazi za kiufundi kama kutengeneza madawati na ujuzi kuhusu masuala mengine,” akasema Bw Cheboi.

Mwenyekiti wa kamati ya Bajeti Kanini Kega naye alisema mradi huo hausuluhishi tatizo la ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana na unafaa kubadilishwa ili ule wa kudumu ukumbatiwe.