Habari

Wabunge wataka mkaguzi apekue Murkomen, Orengo

July 5th, 2019 2 min read

Na DAVID MWERE

WABUNGE walianza likizo fupi Ijumaa lakini baada ya kupitisha hoja ya kumtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Edward Ouko, kuchunguza uhalali wa pesa zinazotumiwa kugharimia afisi za kiongozi wa wengi na kiongozi wa wachache katika Seneti.

Afisi hizo zinashikiliwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Siaya James Orengo, mtawalia.

Haya yanajiri huku vita vya ubabe kati ya mabunge hayo mawili vikiendelea kushamiri huku Seneti ikitisha kuwasilisha kesi kortini kupinga uhalali wa sheria 20 zilizopitishwa na Bunge la Kitaifa bila mchango wa maseneta.

Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki amehusishwa katika vuta nikuvute hiyo baada ya Bunge la Kitaifa kumtaka kutoa ushauri kuhusu wajibu wa Seneti katika mchakato wa utungaji wa sheria.

Vilevile, wabunge wanamtaka Bw Kariuki kutoa ushauri wa kisheria kuhusu pesa ambazo zimetumiwa na maseneta kinyume cha sheria kushughulikia masuala ambayo yako chini ya majukumu ya Bunge la Kitaifa.

Hoja hiyo iliyopitishwa kwa kauli moja, ilidhaminiwa na kiongozi wa wengi Aden Duale na kiongozi wa wachache John Mbadi.

Ilihusu mtindo wa Seneti kuingilia majukumu ya Bunge la Kitaifa kupitia, kwa mfano, kuwaita mawaziri ambao wizara zao hazihusiani na shughuli za kaunti kufika mbele ya Kamati zake.

Mawaziri hao ni kama vile Fred Matiang’i (Usalama), Raychelle Omamo (Ulinzi) na Monica Juma (Mashauri ya Kigeni).

“Tunawaandikia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mwanasheria Mkuu kuuliza ni kwa nini Tume ya Huduma za Bunge (PSC) imebuni afisi katika Seneti ambazo hazitambuliwi na Katiba na ambazo zimekuwa zikifadhiliwa na mlipa ushuru,” Bw Duale akasema.

Aliikashifu Seneti kwa kubuni kamati ambazo zinatekeleza majukumu ambayo yanafanana na yale yanayotekelezwa na bunge la kitaifa.

“Wameanza vita na sasa vita hivi sharti viendelee mpaka mwisho. Ikiwa itabainika kuwa wao hutumia pesa za umma kinyume cha sheria tutawafanyia mchango kuhakikisha kuwa wanalipa pesa hizo,” Duale akasema huku akionekana kuwashambulia maseneta.

Chama chenye wabunge wengi

Kauli ya Mbunge huyo wa Garissa Mjini inatokana na hali kwamba kipengee cha 108 cha Katiba kinasema kuwa kiongozi wa wengi atakuwa kiongozi wa chama chenye wabunge wengi katika bunge la kitaifa.

Na kiongozi wa wachache atakuwa ni kiongozi wa chama chenye wabunge wachache katika bunge lilo hilo.

Hata hivyo, Bw Duale alishangaa ni kwa nini Seneti ilibuni nyadhifa kama hizo na kuishurutisha PSC kuzifadhili kinyume na Katiba au sheria yoyote nchini.