Habari

Wabunge watoa ufafanuzi kuhusu tarehe ya mazishi ya Murunga

November 27th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya muda ya Bunge inayoandaa mazishi ya marehemu mbunge wa Matungu Justus Murunga imefafanua Ijumaa kuwa mazishi yatafanyika Jumamosi, Desemba 5, 2020, wala sio Jumamosi, Novemba 28.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, wanachama wa kamati hiyo wamesema kuwa mwili wa mwendazake utasafirishwa kwa ndege kutoka hifadhi ya maiti ya Lee Funeral Home, Nairobi alfajiri Desemba 5.

“Mwili huo utafasirishwa moja kwa moja hadi boma lake la kwanza katika eneo la Makutano kijiji cha Mautuma, eneobunge la Lugari. Utakaa hapo kwa saa chache kabla ya kusafirishwa tena kwa mazishi nyumbani kwake katika kijiji cha Makunda, eneobunge la Mutungu mwendo wa saa nane alasiri,” akasema Bw Wangwe ambaye pia ni Mbunge wa Navakholo.

Kiranja wa wengi katika Bunge la Kitaifa Emmanuel Wangwe ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya muda ya bunge kuhusu maandalizi ya mazishi ya Justus Murunga amefafanua kuwa tarehe ya mazishi ni Jumamosi, Desemba 5, 2020. Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Ijumaa Novemba 27, 2020 Wangwe amepuuzilia mbali habari zinazoenea kwamba mazishi ni Jumamosi, Novemba 28, 2020. Picha/ Charles Wasonga

Akasisitiza: “Hii ndiyo tarehe ambayo familia na sisi wabunge tumekubaliana kwamba ndugu yetu Murunga atapewa heshima zake za mwisho. Wale wanaosema kuwa mazishi ni kesho Jumamosi (Novemba 28) wanapotosha na ni muhimu wapuuziliwe mbali.”

Aliandamana na wanachama wa kamati hiyo Benjamin Washiali (Mbunge wa Mumias Mashariki), Christopher Aseka (Khwisero), Elsie Muhanda (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kakamega) na Seneta Maalum Petronila Were.

Bw Wangwe amesema ibada ya mazishi ifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Makunda, iliyoko umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwa mwendazake ambako maiti yake itazikwa.

Wabunge hao walifafanua kuwa masharti yote ya kuzuia msambaa wa virusi vya corona yatazingatiwa wakati wa mazishi ya marehemu Murunga.