Na CHARLES WASONGA
WABUNGE Alhamisi alasiri walivuruga shughuli za bunge wakilalamikia hatua ya Hazina ya Kitaifa kuchelewesha utoaji wa Fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF).
Wabunge hao pia walitisha kutopitisha Bajeti ya Ziada ikiwa pesa hizo hazitatumwa kwa maeneobunge yote 290 “haraka iwezekanavyo.”
Badala ya kuingia ukumbini kuendesha shughuli za bunge, viongozi hao waliamua kuketi katika eneo la kuwapokea wageni huku wakiimba “Bila NG-CDF, hakuna vikao, Bila NG-CDF hakuna bajeti ya ziada”.
Hii ni licha ya kwamba kengele ya kuwaita waingie bungeni ilikuwa imelia kwa zaidi ya dakika 20 kinyume cha utaratibu wa kawaida wa kengele hiyo kupigwa kwa dakika 10 pekee.
Juhudi za kiranja wa wengi Maoka Maore na mwenzake Junet Mohammed (Kiranja wa wachache) kuwasihi wabunge kuingia ukumbini ziliambulia patupu huku wabunge wakiitaka hakikisha kuwa pesa hizo zitatumwa katika akaunti za maeneo bunge yao.
“Hatuwezi kushiriki shughuli za leo (Alhamisi) kabla ya Serikali ya Kitaifa kupitia Hazina ya Kitaifa kutupa hakikisho kuwa pesa za NG-CDF zitatolewa. Sasa wanataka tuende kujadili nini bila NG-CDF. Tutawaambia wakazi wa maeneo bunge yetu nini tukienda nyumbani kwa likizo fupi?” akauliza Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma.
Mgomo huo wa wabunge ulisababisha kikao cha alasiri kusitishwa mapema ilhali wabunge walikuwa wameratibiwa kujadili Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORB).
Hii ni baada ya Mbunge wa Tigania Magharibi John Mutunga kuarifu Spika Justin Muturi kuwa hakukuwa na idadi tosha ya wabunge ukumbini kuwezesha shughuli kuendelea kwa mujibu wa sheria.
Kulingana na sheria za bunge kunahitajika angalau wabunge 50 kati ya 349 ili bunge liweze kuendesha shughuli zake rasmi. Lakini Alhamisi alasiri, kulikuwa na wabunge 30 pekee ukumbini.
Wabunge wanadai kuwa kufikia mwezi huu kila eneo bunge limepokea Sh16 milioni pekee kati ya Sh100 milioni ambazo zilipaswa kupokea katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.
Hii ni licha ya kwamba imesalia miezi mitatu pekee kabla ya mwaka huu wa kifedha kufikia kikomo.