Habari Mseto

Wabunge: Wezi wa pesa za Covid wakamatwe

November 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE sasa wanashinikiza wahusika wakuu katika sakata ya Sh7.8 bilioni iliyokumba Mamlaka ya Kusambaza Dawa Nchini (Kemsa) wachukuliwe hatua za kisheria.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Amos Kimunya na mwenzake wa wachache John Mbadi wabunge hao walikashifu asasi zinazochunguza sakata hiyo kwa kujivuta kinyume na agizo la Rais Uhuru Kenyatta.

“Ni zaidi ya siku 100 tangu Rais Uhuru Kenyatta alipoamuru Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kukamilisha uchunguzi wa sakata hiyo baada ya siku 21. Lakini mpaka sasa wahusika hawajatiwa mbaroni ilhali Wakenya na haswa madaktari wanaendelea kuuawa na Covid-19,” akasema Bw Kimunya ambaye ni mbunge wa Kipipiri.

Naye Bw Mbadi alirejelea tukio la Jumatano ambapo Mbunge Seme James Nyikali na wenzake Sarah Korere (Laikipia Kaskazini) na Joyce Emanikor (Mbunge Mwakilishi, Turkana) walitokwa na machozi baada ya kuguswa na masaibu ya wahudumu wa afya akisisitiza kuwa ufisadi katika sekta ya afya unapasa kuzimwa kabisa.

“Kati ya zaidi ya wahudumu 200 wa afya ambao wamefariki kutokana na Covid-19 inasikitisha kuwa 20 miongoni mwao ni madaktari. Hali hii inakera na ndio maana ndugu yangu Nyikal na wenzake walilia jana (Jumatano) walipoelezea shida ambazo wataalamu hawa wanapitia,” akasema Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Wawili hawa, na wabunge wengine, walikuwa wakichangia mjadala kuhusu Hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta kuhusu Hali ya Taifa aliyotoa bungeni Alhamisi wiki jana.

Mnamo Jumatano kioja kilishuhudiwa katika Kamati ya Bunge kuhusu Afya baada ya Dkt Nyikal na wenzake wawili kuangua kilio kutokana na madhila yanayokumba madaktari wakati huu wa janga la corona.

Walizidiwa na hisia baada ya kuguswa masaibu ambayo madaktari na wahudumu wengine wa afya hupitia katika vita dhidi ya corona.

Masimulizi hayo yalitolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Chibanzi Mwachonda ambaye alisema madaktari wanafariki kwa wingi kwa kukosa bima ya afya, mishahara bora na marupurupu hitajika licha ya kuhatarisha maisha yao wakiwahudumia wagonjwa wa Covid-19.

“Ningetamani kuwa mkutano huu ungekuwa ukifanyika katika Ikulu na kuongozwa na Rais ili wale ambao humshauri wasikie moja kwa moja,” akasema Dkt Nyikal.

Akaongeza, “Hao ndio watu ambao wanapasa kusikiza maelezo haya kutoka kwa madaktari. Ninakerwa mno. Hii si haki.”

Mbunge huyo wa Seme amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Katibu katika Wizara ya Afya wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Dkt Nyikal pia alilalamikia hali mbaya ya hospitali za umma ambapo wahudumu wa afya wanafanyakazi bila vifaa kinga (PPEs), hali ambayo inahatarisha maisha yao.

Jana, wabunge kutoka mirengo yote miwili waliitaka Wizara ya Afya kuamuru PPEs za thamani ya Sh6.2 bilioni zilizonunuliwa na Kemsa kwa bei ghali mnamo Aprili zisambaziwe wahudumu wa afya bila malipo.