Habari MsetoSiasa

Wabunge wote wanafaa kujitenga – Murungi

April 8th, 2020 1 min read

DAVID MUCHUI NA FATUMA BUGU

Mbunge wa Imenti Kusini, Kathuri Murungi amewataka wabunge wote kuenda karantini akidai kuwa walijumuika na mbunge ambaye alitoka Uingereza.

Kupitia mtandaoni, Bw Murungi alieleza jinsi wabunge kadhaa walivyotoka Uingereza na kwenda moja kwa moja hadi bungeni na kujumuika na wenzao.

Alidai alipatwa na dalili za malaria Alhamisi iliyopita, hali iliyomlazimu kwenda hospitalini haraka ambapo alipatikana kuwa na maambukizi ya damu.

Kulingana naye, alijumuika na wafanyikazi wenzake na ndipo alikata shauri kwenda kufanyiwa uchungzui wa virusi vya corona katika Hospitali ya Aga Khan, Jijini Nairobi.

“Nakumbuka nilimuona mfanyikazi mmoja akiwa amekaa lakini akiwa na wasiwasi…..vipimo vilipelekwa katika maabara ya KEMRI. Niliwaona wauguzi wakiwa na hofu yakunihudumia, hawakuwa na uhakika na hali yangu, ” alisema mbunge huyo.

Hivyo basi nilipelekwa karantini ya lazima katika hospitali ya Aga Khan baada ya kuwaeleza juu ya kujuimuika kwake na mbunge aliyetoka Uingereza.

“Nilitaka tu kufahamu hali yangu na ya familia yangu, ” alisema mtandaoni.

Mbunge huyo alijitenga kuanzia Jumapili hadi Alhamisi mchana baada ya KEMRI kuhakikisha kutodhurika kwake na virusi vya corona.

“Nawahusia wafanyikazi wenzangu kujitenga kwa siku 14, na ikiwezakana kufanya vipimo ili kujua iwapo wamedhurika na virusi hivyo na mapema, ” alisema Bw Murungi.

Pia aliwataka Wakenya kufuata hatua za kukabiliana na janga la corona zilizotolewa ili kuepuka uenezaji zaidi.

Familia yake imetoa Sh100,000 za kuweka vifaa vya kuosha mikono kwenye masoko ya Imenti.