Habari za Kitaifa

Wacha kudanganya na usahau UDA, maafisa wamjibu Malala


WAANZILISHI wa United Democratic Alliance (UDA), wamepuuza kauli iliyotolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Cleophas Malala kwamba alifurushwa kwa kutetea Naibu Rais Rigathi Gachagua asitimuliwe mamlakani, wakiitaja kama uongo na kuapa kumtimua kama mwanachama wa chama hicho.

Wakiongozwa na Joe Khalende, waanzilishi hao walisema katika taarifa kwamba madai ya Bw Malala kwamba angali katibu mkuu wa chama ni ya uongo.

“Waanzilishi wa UDA wanasisitiza kwamba wanaunga mkono kwa dhati mabadiliko yaliyofanywa katika chama kwa kumteua Hassan Omar kama Kaimu Katibu Mkuu na kumshauri Malala akomeshe mawazo potovu kuhusu yaliyopita,” Bw Khalende alisema katika taarifa.

Haya yalijiri saa chache baada ya Bw Malala kudai kuwa kuondolewa kwake hakukuwa halali na kunahusishwa na mipango ya kumuondoa ofisini Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Chama hicho kimesema kuwa taarifa ya Bw Malala imethibitisha hofu yao kuu kwamba amekuwa akifanya kazi na watu wasio na nia njema ili kuhujumu chama kutoka ndani.

Huku Bw Malala akipinga kuondolewa kwake, chama hicho kimewaonya maafisa wa chama dhidi ya kujihusisha naye.

“Pia tunamuonya dhidi ya kutumia nembo ya chama kutuma taarifa kwa vyombo vya habari. Tunachukua fursa hii mapema kutahadharisha wafanyakazi dhidi ya kujihusisha au kufanya shughuli yoyote na Bw Malala.”

Bw Khalende alidai kuwa wakati wa uongozi wa Bw Malala, chama hicho kilikumbwa na uhuni wa kisiasa, na usimamizi mbaya wa raslimali za chama.

Chama hicho kiliendelea kusema kwa kufichua uhusiano wake na Bw Gachagua, Bw Malala alianika juhudi zake za siri za kuhujumu ajenda ya kiongozi wa chama hicho, Rais William Ruto.

Viongozi hao walipuuza madai ya Malala dhidi ya mwenyekiti wa chama Cecil Mbarire na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa kwamba wawili hao walikuwa wakipanga njama ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua.

“Waasisi na mamilioni ya wanachama wa chama hawataruhusu amani na utulivu unaopatikana kwenye chama kuvurugwa na wanasiasa walioshindwa uchaguzini wanaojitafuta maslahi yao ya kibinafsi. Waanzilishi wa UDA wamekuwa wakitilia shaka tabia ya Malala, mienendo ya uongozi, maamuzi na uaminifu wake.”

Waliapa kushinikiza kufukuzwa kwa Bw Malala kutoka chama hicho miongoni mwa hatua zingine kupitia Kamati ya Kusuluhisha Mizozo ya Ndani ya chama.

Bw Malala aliahidi kutoa ripoti ambayo itafichua kwa kina jinsi baadhi ya maafisa wa chama hicho walikuwa wakipanga kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua.