Michezo

Wachanganuzi washikilia ‘Ndovu’ Arsenal hawatabeba taji la EPL licha ya sare na Man City

April 2nd, 2024 2 min read

MANCHESTER, UINGEREZA:

ARSENAL wangali nyuma ya viongozi Liverpool na mabingwa watetezi Manchester City katika orodha ya timu zinazopigiwa upatu kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, licha ya kuongeza asilimia 5.8 baada ya kugawana alama na Man-City wikendi.

Wachanganuzi wa data za michezo Opta wanaamini vijana wa kocha Jurgen Klopp wamekaa pazuri kuponyoka na taji, wakiwa na asilimia 47.7 baada ya kujiongezea asilimia 12.4 kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Brighton.

Nao Man-City na Arsenal walishuhudia kibarua kikiongezeka walipodondosha alama Jumapili jioni.

Kulingana na uchanganuzi wa data kupitia kompyuta Supercomputer, Man-City ya kocha Pep Guardiola wamepoteza asilimia 12.4 na sasa wana 33.5.

Nao Gunners chini ya ukufunzi wa Mikel Arteta wameimarika kutoka asilimia 13.0 hadi 18.8 .

Zikisalia mechi tisa, Liverpool wana alama 67 kisha Arsenal (65), City (64), Aston Villa (59), Totteham (56) na Manchester United (48) katika nafasi sita za kwanza.

Arsenal wataalika Luton Town (18) nao City watavaana na Villa hapo kesho, mtawalia. Liverpool pia watakuwa nyumbani katika mchuano ujao dhidi ya Sheffield United (20), Alhamisi.

Vijana wa Guardiola, ambao ni mara ya kwanza katika mechi 58 za nyumbani walishindwa kufunga bao, wanafukuzia taji la nne mfululizo la ligi.

“Tunapokuwa kileleni, sisi huwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa. Taji lilikuwa mikononi mwetu, lakini sasa halipo,” akasema Guardiola ambaye vijana wake walikuwa wamepepeta Arsenal mara nane katika mashindano yote ugani Etihad kabla Jumapili.

Kwa upande wake, Arteta alifurahia pointi moja.

“Tulilinda ngome yetu vizuri sana…Ni mara ya kwanza City hawajapata bao nyumbani kwa miaka mitatu. Hata hivyo, sijafurahia kuwa hatukutumia nafasi nzuri tulipata kufunga bao. Siwezi kuwa na furaha kabisa,” akaongeza Mhispania huyo.

Leverkusen taji lanukia Ligi Kuu ya Ujerumani

Nao Bayer Leverkusen wananusia taji la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kufungua mwanya wa alama 13 dhidi ya nambari mbili na mabingwa watetezi Bayern Munich.

Leverkusen walikamata nafasi ya pili 1996-1997, 1998-1999, 1999-2000, 2001-2002 na 2010-2011, lakini hawajawahi kutawala ligi hiyo ambayo Bayern wanashikilia rekodi ya mataji 33 yakiwemo 11 mfululizo.

Vijana wa kocha Xabi Alonso watakuwa timu ya 30 kushinda Bundesliga iwapo watavuna pointi tisa kutoka kwa mechi saba zilizosalia.

Leverkusen wamezoa ushindi mara 23 na kupiga sare nne. Ni timu pekee katika ligi hiyo ya klabu 18 ambayo haijapoteza msimu huu.

Leverkusen walishinda mechi yao ya nane mfululizo ligini kwa kuzaba Hoffenheim 2-1 ugani BayArena.

“Tunakabiria kutimiza lengo letu kubwa,” Alonso akasema baada ya ushindi dhidi ya Hoffeheim, saa chache kabla ya kunufaika na Bayern ya kocha Thomas Tuchel kupoteza 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund ugani Allianz Arena.