Habari MsetoSiasa

Wachezaji densi waliomtumbuiza Moi wadai Kibaki aliwadharau

February 10th, 2020 2 min read

NA VITALIS KIMUTAI

HUKU Wakenya wakijiandaa kwa ibada ya mwisho ya Rais Mstaafu Daniel Arap Moi, wanachama wa kundi la wasakataji ngoma za kitamaduni kutoka Bomet wameeleza jinsi Rais aliyefuata, Mwai Kibaki, alivyowapuuzilia mbali walipotaka kumtumbuiza.

Kundi hilo kwa jina Konoin lilikuwa limetumbuiza Marais kwa zaidi ya miaka 50, tangu Jomo Kenyatta, Daniel Arap Moi, Mwai Kibaki na sasa linasema humtumbuiza Rais Uhuru Kenyatta.

Waliwaburudisha viongozi hao katika Ikulu za Nairobi, Nakuru, Mombasa na katika nyuga za Nyayo, Kasarani na Afraha pamoja na makazi ya Mzee Kenyatta na Mzee Moi yaliyoko Gatundu na Kabarak mtawalia.

Katika mahojiano kuhusu kumbukumbu za Mzee Moi, walisikitika kwamba katika enzi za utawala wa Bw Kibaki, waliumia sana wakati aliwashambulia kwa maneno makali akisema hakuwa na muda wa kujiburudisha kwa nyimbo na densi zao.

“Siku moja akiwa katika eneobunge la Konoin, Kaunti ya Bomet, Bw Kibaki alitufokea akitutaja kama watu wavivu na wawindaji wa ngozi za wanyama pori waliotumia ngozi za wanyama kama mavazi,” akasema Mzee Samwel Korgoren, 78, ambaye ni mwanachama wa kundi hilo.

Hata hivyo, Taifa Leo haingeweza kuthibitisha madai haya kwa njia huru. Wasakataji ngoma hao 48 wakongwe walimsifia mwendazake Mzee Moi ambaye walidai alifahamu nyimbo zao na kila mara aliutaja hata wimbo aliotaka achezewe.

“Kati ya marais wote ambao tumewaburudisha, Mzee Moi alikuwa mpenda nyimbo zetu na alikuwa akijumuika nasi jukwani kusakata densi,” akasema Bw David Sigei, mwanachama wa kundi hilo.

Mzee Kipkirui, 83 naye alifichua kwamba Mzee Moi alikuwa na raha na hukuficha furaha yake akitumbuizwa vyema.

Wazee hao walikumbuka jinsi kundi lao lilivyokuwa maarufu wakati wa utawala wa Mzee Moi na kila mara walisafirishwa kwa mabasi ya shule au matatu kumburudisha Mzee Kenyatta nyakati za jioni.

“Tulimtumbuiza Mzee Kenyatta hadi nyakati za usiku lakini hatukuwahi kumkaribia. Kulikuwa na walinda usalama waliomzingira na kutoa ulinzi mkali,” akasema Mzee Chepkulu Chepkeiyo.

Mwanachama wa kundi hilo Mzee Tirinus Rotich, naye anakumbuka mshikemshike uliotokea walipokuwa wakimtumbuiza Mzee Kenyatta katika uwanja wa Afraha, Nakuru.

“Tukiwa tunamtumbuiza Mzee Kenyatta, kulitokea mlipuko mkubwa na kila mtu akatimka mbio huku Rais akibebwa na walinzi wake na kuondolewa uwanjani humo,” akasema Mzee Rotich.

“Kila mtu aliamini lilikuwa bomu lililotegwa chini ya ardhi lakini ilibainika baadaye kwamba kwamba ni gurudumu la lori ndilo lilipasuka,” akaongeza.

Walikuwa kati ya wapigaji ngoma za kitamaduni waliomtumbuiza Mzee Kenyatta mnamo Juni 1, 1978 ugani Afraha kabla ya Rais huyo kufariki Agosti 22, mwaka uo huo.