Michezo

Wachezaji mahiri lakini bado hawajashindia klabu zao taji

September 17th, 2020 6 min read

Na GEOFFREY ANENE

NI ndoto ya kila mchezaji kupata ufanisi na klabu na nchi yake. Wakati mwingine anafaulu kutimiza ndoto hii katika klabu pekee ama timu ya taifa pekeeama katika majukwaa hayo yote mawili ama kuambulia pakavu katika klabu na pia nchi.

Ukumbi huu unaangazia majina makubwa katika michezo ya Kenya ambayo yamepata mafanikio yakipeperusha bendera ya Kenya, lakini hayana taji la ligi.

GRIFFIN LIGARE

Ligare ni mmoja wa wachezaji matata katika timu ya taifa ya mpira wa vikapu almaarufu Morans. Mchezaji huyu anafahamika kwa mchezo wa kasi ya juu na chenga kali. Alisherehekea kufikisha umri wa miaka 35 mnamo Mei 19 mwaka huu.

Ligare amewakilisha Kenya katika mashindano mengi ya kimataifa yakiwemo yale ya Bara Afrika (AfroCan) mwaka 2019 mjini Bamako nchini Mali ambako Morans ilijizolea umaarufu mkubwa kwa kuvuna medali ya fedha.

Morans, ambayo haikupigiwa upatu kabisa wa kutikisa katika mashindano hayo, ilipoteza michuano miwili pekee, yote dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – katika mechi za makundi na katika fainali. Iliduwaza Nigeria, Ivory Coast, Tunisia na Morocco.

Ligare amekuwa mchezaji wa klabu ya Thunder tangu mwaka 2009. Mchezaji huyu ndiye mchezaji nyota katika timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Mpira wa Vikapu Kenya.

Ligare amekuwa akifunga kati ya alama 20 na 30 katika kila mechi ligini, lakini hajawahi kubeba ubingwa wa ligi hiyo. Mara nyingi, Thunder, ambayo ni klabu ya kujitegemea, imepigwa breki katika hatua ya robo-fainali.

Hata hivyo, Thunder imeonyesha kuimarika katika misimu miwili iliyopita ilipokamilisha kampeni yake katika nafasi ya tatu mwaka 2018 na kuridhika katika nafasi ya pili mwaka 2019 nyuma ya Ulinzi Warriors.

“Matokeo yetu ya mwaka 2019 yanasalia kuwa mazuri katika historia ya klabu ya Thunder. Tunaamini bado tuna pumzi ya kutosha kujaribu kutafuta taji msimu huu ama tuanze kujijenga upya.

“Tumekuwa tukitatizika katika mechi za baada ya msimu wa kawaida za kutafuta mshindi kwa sababu zinafuatana kwa karibu na tunalazimika kusafiri nje ya Nairobi huku tukihitajika kupatia wachezaji marupurupu ya kufanya mazoezi na pia ya kucheza mechi. Sisi tunajitegemea kwa hivyo inahitaji kujitolea sana.

Tunajaribu kujipanga vyema kuhakikisha tunapita kizuizi hiki kwa kuweka mikakati bora,” anasema mwalimu huyo wa mazoezi ya viungo kutoka Shule ya International School of Kenya (ISK) mjini Nairobi.

Ligare alihudhuria Shule ya Msingi ya Garrison mjini Nanyuki na Shule ya Upili ya Siliti mjini Laikipia kabla ya kusomea Digrii ya Sayansi ya Michezo katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

PHILIP MAIYO

Hakuna mchezaji amevuma duniani katika voliboli kutoka Kenya kama Maiyo. Mchezaji huyu mwenye urefu wa mita mbili alistaafu uchezaji 2019.

Maiyo alichezea klabu ya Majeshi (KDF) na Benki ya KCB humu nchini. Alianza uchezaji wa voliboli KDF, akajiunga na KCB wakati timu ya KDF ilivunjwa na tena akarejea KDF ilipofufuliwa. Hakushinda ligi na klabu hizo.

Alijitosa katika voliboli ya malipo ughaibuni na kucheza katika mataifa ya Bulgaria, Romania, Uturuki, Lebanon, Qatar na Japan kabla ya kustaafu.

Maiyo sasa anajihusisha na ukufunzi. Tovuti ya Trendcelebsnow.com inasema Maiyo ndiye mchezaji tajiri wa voliboli nchini Kenya. Inakadiria ukwasi wake kuwa kati ya Sh107 milioni na Sh532 milioni.

Maiyo,38, ambaye alikuwa mshambuliaji hodari enzi zake, ni naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli Kenya tawi la North Rift.

Maiyo, ambaye dadake Lydia Maiyo pia alichezea timu ya taifa ya wanawake ya Malkia Strikers, anatoka katika kaunti ya Nandi.

Kaunti hiyo, ambayo inafahamika sana kwa wanariadha mastaa akiwemo mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42 Eliud Kipchoge, pia inajivunia wanavoliboli matata kama seta Brian Melly na mshambuliaji Cornelius Kiplagat (GSU) na seta Kelvin Kipkosgei na mshambuliaji Timon Kimutai (Kenya Prisons).

Kwa wakati huu, wachezaji hawa wanne wanachezea timu ya taifa ya wanaume ya Kenya. Kocha mkuu wa Malkia Strikers Paul Bitok, ambaye pia ni mshauri wa kiufundi wa klabu ya kinadada ya KCB, anatoka katika kaunti ya Nandi.

“Maiyo alikuwa mchezaji aliyejitolea kwa dhati katika uchezaji wake. Alipenda kufanya mazoezi ambayo matunda yake yalionekana wakati wa mechi. Kwake nidhamu ilikuwa maisha yake.

“Alikuwa na nidhamu ya kutosukumwa. Alipenda nchi yake. Alikuwa na motisha kila alipoitwa kuchezea timu ya taifa. Alikuwa mpenda amani. Kama kocha wake, nampatia alama 10 kwa 10. Anasalia kuwa mchezaji anayeigwa na wachezaji wengi wanaojitosa katika voliboli. Namtakia kila la heri katika uongozi wake wa voliboli,” anasema kocha mtajika Moses Epoloto.

NDUGU WA EMONYI

Nyota wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya Humphrey Kayange, Collins Injera na Michael Agevi hawajawahi kushinda Ligi Kuu (Kenya Cup).

Kayange na Injera walichezea klabu ya Ulinzi iliyovunjwa kabla ya kuwajibikia Mwamba kwa miaka mingi. Ndugu hao wa Emonyi wamechezea timu za taifa za Shujaa na Simbas. Kayange,37, ni nahodha wa zamani wa Shujaa.

Mwanafunzi huyu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) ni mwakilishi wa wanamichezo katika Kamati ya Olimpiki Kenya baada ya kustaafu Oktoba 2016. Injera, 33, ni mfungaji wa miguso mingi kwenye Raga ya Dunia nyuma ya Muingereza Dan Norton.

Mwanafunzi huyu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Daystar amefungia Kenya miguso 271 tangu aanze kuichezea mwaka 2006 katika duru ya Dubai.

Aliingia katikadaftari za kumbukumbu kuwa mfungaji wa miguso mingi kwenye Raga ya Dunia alipovunja rekodi ya raia wa Argentina Santiago Gomez Cora ya miguso 230 katika duru ya London mwaka 2016.

Norton anashikilia rekodi hiyo baada ya kupiku Injera katika duru ya Hong Kong mwaka 2017. Kayange na Injera walikuwa katika kikosi cha Shujaa kilichonyakua taji la duru ya Singapore mwaka 2016.

Wameshiriki Kombe la Dunia la wachezaji saba kila upande na michezo ya Jumuiya ya Madola. Pia, walishiriki Michezo ya Olimpiki mwaka 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil. Agevi pia amewakilisha Kenya kimatafa akichezea Shujaa kwenye Raga ya Dunia.

Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 28 ni kocha katika akademia ya Mpesa Foundation. Injera na Agevi bado wanachezea klabu ya Mwamba ambayo imeshinda ligi mara moja, mwaka 1983. Ulinzi haikushinda ligi.

NIXON NYANGAGA

Nyangaga alianzisha klabu ya Greensharks mwaka 2002 akishirikiana na Patrick Ogara, Richard Ochieng’, John Mark Otiato, Walter Onyango, David Olalo na Job Omach. Greensharks inashiriki Ligi Kuu ya Mpira wa Magongo. Nyangaga amewahi kuwakilisha Kenya kimataifa.

Alikuwa katika timu iliyofuzu kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1998, ingawa hakuwa kikosini wakati wa michezo hiyo mjini Kuala Lumpur, Malaysia.

“Nilipata ujuzi mkubwa kuchezea Greensharks, inayolenga kukuza wachezaji wanaoweza kukabiliana na maisha hata nje ya uchezaji. Sikushinda Ligi Kuu, lakini tulikaribia sana mwaka 2009 tulipokamilisha katika nafasi ya pili. Tunakabiliwa na changamoto nyingi kwa sababu sisi tunajitegemea.

Changamoto zenyewe zinajumuisha kulipia uwanja wa kufanyia mazoezi, kupatia wachezaji nauli na pia kuhakikisha wanapata mahali pa kulala tunaposafiri kwa mechi nje ya Nairobi,” anasema Nyangaga,47, ambaye sasa ni mkurugenzi wa kiufundi wa Greensharks.

Nyangaga alisomea Shule ya Upili ya Kisumu Day iliyofahamika kukuza talanta ya hali ya juu ya mpira wa magongo miaka iliyoenda.

Baada ya kukamilisha Shule ya Pili, Nyangaga alijiunga na Chuo cha Anuai cha Mombasa. Yeye sasa ni mwalimu wa mazoezi ya viungo katika Shule ya ISK. Amejifunza pia masuala usimamizi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Kiungo wa Greensharks Leon Magomere pia aling’ara akichezea Kenya mara kadha, lakini hajawahi kushinda ligi.

NDUGU WA WANYAMA

Mwanasoka McDonald Mariga Wanyama, ambaye ni mwanasiasa, alivalia jezi za klabu za Tusker na Kenya Pipeline kwenye Ligi Kuu ya Kenya kati ya mwaka 2003 na 2005.

Hakushinda ligi hiyo, lakini alijiundia jina Ulaya, hasa nchini Italia alikochezea Inter Milan chini ya kocha Jose Mourinho na Parma.Mariga pia alisakata soka ya malipo nchini Uswidi na Uhispania alikokamilisha uchezaji wake katika klabu ya Real Oviedo mwaka 2018.

Mariga,33, ni Mkenya wa kwanza kushiriki Klabu Bingwa Ulaya. Alifanya hivyo akiwa Inter Milan msimu 2009-2020. Inter ilishinda Klabu Bingwa Ulaya msimu huo.

Victor Mugubi Wanyama,29, alichezea Nairobi City Stars na AFC Leopards kwenye Ligi Kuu ya Kenya kabla ya kuyoyomea Uswidi, Ubelgiji, Scotland na Uingereza alikokuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Ligi Kuu ya EPL akichezea Southampton. Mugubi alijiunga na Montreal Impact inayoshiriki Ligi Kuu ya Amerika na Canada (MLS) akitokea Tottenham Hotspur mnamo Machi 3, 2020.

Viungo hawa wawili wamewakilisha Kenya kimataifa mara nyingi tu. Hawajashinda chochote na Harambee Stars na pia hawakushinda ligi humu nchini. Mugubi alikuwa nahodha wa Stars wakati wa Kombe la Bara Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri.

VIRGINIA MUIGAI

Mwanafunzi huyu wa zamani wa shule za upili za Tetu na Katikamu SDA na vyuo vikuu vya Nkumba, Dedan Kimathi na Mount Kenya alicheza voliboli Blue Triangle na KCB.

Timu hizi mbili hazijawahi kuibuka bingwa wa ligi. Muigai alikuwa mshambuliaji wa pembeni kushoto. Alistaafu akiwa na umri wa miaka 26 mwaka 2014 wakati waajiri wake, kampuni ya simiti ya East African Portland iliamua kujiondoa katika michezo.

“Kupata namba katika timu ya taifa haikuwa rahisi enzi yangu. Ushindani ulikuwa mkali ajabu. Ingawa sikushinda ligi, ni katika ligi nilikopata fursa ya kupimana na wachezaji mahiri kama Jane Wacu ambaye pia alisomea Tetu, Lydia Maiyo na Esther Mwombe.”

Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF), benchi ya kiufundi na wachezaji wenzangu walinisaidia sana na hatimaye nikaimarisha ujuzi wangu. Majukumu ya mwanavoliboli yanahitaji kuwa na ari, kujitolea na pia kuwa na nidhamu ya hali ya juu,” anasema Muigai.

BRENDA NAFULA

Kipa Nafula aliitwa kuchezea timu ya taifa ya mpira wa magongo mara kadha, ingawa hakuweza kumpiku kipa nambari moja Josephine Ataro. Nafula, ambaye aligonga umri wa miaka 40 mwezi uliopita wa Agosti, ni mchezaji wa Mombasa SC. “Mimi hujituma vilivyo uwanjani.

Licha ya kuwa sikushinda ligi, mpira wa magongo unasalia kipenzi changu cha kwanza na kazi ya kulinda lango kuwa kazi ninayopenda.

Kuitwa tu kuchezea timu ya taifa ilikuwa kitu kikubwa wakati wetu,” anasema Nafula, ambaye ni mwalimu wa shule ya chekechea mjini Mombasa na pia anasaidia katika kukuza michezo katika akademia ya Tunza katika kaunti hiyo.

Anaongeza, “Wahenga walisema maisha huanza mtu anapofikisha umri wa miaka 40 kwa hivyo mimi siko tayari kuangika glavu hivi karibuni. Nimejiunga na timu ya wachezaji walio na umri wa miaka 40 na kuendelea.”