Michezo

Wachezaji wa Arsenal wakubali kukatwa mishahara

April 19th, 2020 1 min read

NA CHRIS ADUNGO

WACHEZAJI wa Arsenal huenda wakawa wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kukubali kunyofolewa mshahara baada ya kuahidiwa tuzo za kutamanisha iwapo watafuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Wanasoka wa Arsenal wanatazamiwa kupunguziwa mshahara kwa hadi asilimia 12.5 ambayo watarejeshewa iwapo watafuzu kwa mapambano ya UEFA msimu ujao au wa 2021-22.

Ikiwa Arsenal watajikatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha UEFA muhula ujao, miamba hao wa soka ya Uingereza watapokezwa pia bonasi ya hadi Sh14 milioni.

Isitoshe, kila mmojawapo wa wachezaji wa Arsenal atatia mfukoni kima cha Sh70 milioni kwa kunyanyua ubingwa wa UEFA mnamo 2021 au Sh14 milioni kwa kuibuka wafalme wa Europa League.

Hadi kusitishwa kwa kampeni za EPL msimu huu kutokana na virusi vya homa ya corona, Arsenal walikuwa wakishikilia nafasi ya tisa huku wakisalia na alama nane zaidi nje ya mduara wa nne-bora. Ni michuano 10 pekee imesalia kabla ya msimu wa EPL kutamatika rasmi muhula huu.

Mapema wiki hii, usimamizi wa Arsenal ulifikia maamuzi ya kupunguza hadi thuluthi moja ya mishahara ya wachezaji na wafanyakazi kwa kipindi cha miezi 12 ijayo.

Mijadala ya kibinafsi inaendeshwa na klabu mbalimbali za EPL kwa pamoja na wachezaji wao kuhusu uwezekano wa kupunguza mishahara, hatua ambayo klabu za Newcastle United, Tottenham Hotspur, West Ham United, Bournemouth na Southampton zimepania kukumbatia.

Kwa mujibu wa taarifa ya wamiliki wa Arsenal, kikosi hicho kitakuwa radhi kurejeshea mashabiki wake ada za tiketi za kuhudhuria mechi zilizosalia msimu huu iwapo itaamuliwa kwamba mechi nyinginezo zitandazwe ndani ya viwanja vitupu.