Wachezaji wa Gor Mahia wagoma tena mechi ya CAF ikibisha

Wachezaji wa Gor Mahia wagoma tena mechi ya CAF ikibisha

Na GEOFFREY ANENE

KICHAPO kingine kambini mwa Gor Mahia kwenye mashindano ya Afrika kinanukia baada ya timu hiyo kugoma, mkondo ambao imefuata mara kadhaa na kuishia kubanduliwa ikiwemo dhidi ya Waalgeria CR Belouizdad kwenye Klabu Bingwa Afrika Januari.

Migomo, ambayo ni haki ya wachezaji wanapohisi maslahi yao hayazingatiwi, ilichangia katika mabingwa hao wa Kenya kukung’utwa 6-0 Desemba 2020 jijini Algiers na 2-1 Januari jijini Nairobi katika mechi za kuingia makundi ya Klabu Bingwa.

Vichapo hivyo vilisababisha Gor kuteremshwa hadi mashindano ya daraja ya pili, Kombe la Mashirikisho Afrika (Confederation Cup).

Vijana wa Vaz Pinto wameratibiwa kumenyana na NAPSA Stars hapo Februari 14 uwanjani Nyayo katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kuamua nani ataingia makundi ya Confederation Cup.

Hata hivyo, Gor walianza mgomo Jumatano, siku ambayo NAPSA waliingia nchini.

Hawakufika uwanjani Camp Toyoyo, juku wachezaji wakifichua kuwa wanadai mshahara wa miezi miwili.

Gor ndiyo tegemeo la pekee la Kenya kwenye mashindano ya Afrika msimu 2020-2021. Hii ni baada ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kukosa kuingiza timu katika kipute cha Confederation Cup kufuatia kufutiliwa mbali kwa mashindano ya kufuzu ya Betway Cup mwaka 2020 kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Mshindi kati ya Gor na NAPSA baada ya mechi ya marudiano Februari 21 nchini Zambia, atajihakikishia tuzo ya Sh60.1 milioni za kuingia mechi za makundi.

You can share this post!

Al Duhail anayochezea ‘Engineer’ Olunga...

Man-City yaweka hai matumaini ya kutwaa mataji manne baada...