Michezo

Wachezaji watatu warejea katika kikosi cha Shujaa

February 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HERMAN Humwa, Charles Owino na Michael Agevi wamerejea katika kikosi cha timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande kitakachoshiriki duru mbili zijazo za Raga ya Dunia katika miji ya Las Vegas mnamo Machi 1-3 na Vancouver mnamo Machi 9-10.

Kikosi hicho cha kocha Kocha Paul Murunga kitaelekea nchini Marekani mnamo Februari 23 usiku kikiwa pia kina sura mpya kabisa Edmund Anya.

Wanne hawa wamejaza nafasi za Harold Anduvate na Mark Wandeto ambao wanauguza majeraha na Eliakim Kichoi na William Reeve ambao wamepumzishwa.

Humwa na Owino walishiriki duru mbili za kufungua msimu katika miji ya Dubai na Cape Town mwezi Desemba mwaka 2018. Agevi, ambaye ni ndugu mdogo wa nyota Collins Injera, anarejea kikosini baada ya kuchezea Kenya mara ya mwisho msimu 2014/2015.

Shujaa inashikilia nafasi ya 13 kwa alama 12 kwenye ligi hii ya duru 10. Itamenyana na Marekani, Argentina na Ufaransa zinazoshikilia nafasi ya pili, tisa na 12 mtawalia katika mechi za Kundi B mjini Las Vegas.

Kikosi cha Shujaa kitakachoshiriki Las Vegas Sevens na Vancouver Sevens:

Jacob Ojee, Vincent Onyala, Daniel Taabu, Johnstone Olindi, Brian Wahinya, Bush Mwale, Brian Wandera, Cyprian Kuto, Edmund Anya, Herman Humwa, Charles Owino, Michael Agevi.