Michezo

Wachezaji watishia kugura Chelsea Sarri asipotimuliwa

May 22nd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

BAADHI ya wachezaji wa Mabingwa wa zamani Chelsea wametishia kuondoka klabuni humo iwapo meneja Maurizio Sarri atasalia kama kocha wa kikosi hicho msimu ujao.

Ripoti ndani ya klabu hiyo zinaarifu kwamba baadhi ya wachezaji nyota hawafurahishwi na mbinu za ukufunzi za Mwitaliano huyo licha ya kwamba Chelsea ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Lig Kuu ya Uingereza(EPL) baada ya kukamilika msimu wa 2018/19.

Mashabiki wa klabu hiyo pia wameonekana kukerwa na mbinu za mkufunzi huyo na walimkemea kwenye mechi kadhaa za EPL ikizingatiwa huu umekuwa msimu wake wa kwanza kama mkufunzi wa Chelsea.

Sarri hasa alijipata matatani mbele ya mashabiki baada ya kufungwa 6-0 na Mancity Februari 10, 2019 ingawa alibadilisha hali baadaye na Chelsea ikaanza kusajili matokeo ya kuridhisha katika mechi zilizofuatia.

Hata hivyo, duru zinaeleza kwamba uongozi wa Chelsea ushaamua kuagana na kocha huyo wa zamani wa Napoli bila kujali iwapo atapata ushindi au la kwenye fainali ya Ligi ya Uropa dhidi ya Arsenal Mei 29.

Jagina wa klabu hiyo Frank Lampard na meneja anayeondoka wa Juventus ya Italia, Massimiliano Allgeri ni kati ya wakufunzi mahiri waliotajwa kuwa katika mstari wa mbele kuchukua nafasi ya Sarri.