Habari

Wachezaji wawili waliopatikana na hatia ya ubakaji kuhukumiwa Ijumaa ijayo

August 9th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE na SAM KIPLAGAT

WACHEZAJI wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya, Alex Mahaga Olaba na Lawrence Frank Wanyama wanakodolea macho kifungo cha jela kisichopungua miaka 15 baada ya mahakama mnamo Alhamisi kuwapata na hatia ya kubaka mwanamuziki mmoja.

Olaba na Wanyama, ambao awali walikuwa wamepinga madai ya ubakaji na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000, walitarajiwa kujua hukumu dhidi yao leo Ijumaa, lakini ikaahirishwa hadi Ijumaa, Agosti 16, 2019.

Wakijitetea mbele ya hakimu Martha Mutuku katika mahakama jijini Nairobi, wawili hao wamesema wangali vijana kiumri ambao wanahitaji kujijenga kimaisha.

Hata mmoja wao amesema alikuwa amepata nafasi ya kusoma – scholarship – lakini kesi hiyo inaelekea kuzima ndoto yake.

Nao upande wa mashtaka umesema wawili hao walichukua sherehe ya mwanadada kuigeuza raha kuwa karaha kwa kutekeleza unyama dhidi yake.

Kiongozi wa mashtaka Bi Everlyn Onunga ameomba ubakaji utangazwe kuwa ni janga la kitaifa.

Mwanamke huyo, ambaye jina lake limebanwa kwa sababu za kiusalama, alishtaki wachezaji hao kutoka klabu ya Kenya Harlequin kwa kumbaka usiku kucha kuanzia hafla ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Februari 10, 2018, na mkesha wa Februari 11, 2018, katika majumba ya Seefa mtaani Highrise jijini Nairobi.

Alipata mimba baada ya kisa hicho na kudai kuwa mmoja wa wachezaji hao alitisha kumpeleka mahakamani akitangazia umma kisa hicho.