Habari Mseto

Wachimba mawe walia kuteswa

July 22nd, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAFANYAKAZI  37 katika matimbo ya mawe eneo la Juja, Kiambu wanalalamika kudhulumiwa na mwajiri wao.

Wafanyakazi hao walisema kampuni hiyo ya Goldenson Construction Cop Ltd, imekuwa ikiwatesa bila huruma.

Bw David Okello mmoja wa wafanyikazi wa kampuni hiyo anasema kuwa mmiliki wa kampuni hiyo ni mchina ambaye amekuwa na kiburi huku akiwapiga wafanyi kazi wake kama watoto.

“Ni hivi mwishoni mwa wiki wakati nilikuwa nikipakia mawe kwenye lori naye mchina huyo alikuwa akikagua jinsi kazi ilikuwa ikiendeshwa. Kufumba na kufumbua jamaa huyo alianza kunizaba makofi na kunipiga ovyo bila sababu. Baadaye nilianguka sakafuni kwa kishindo,” alisema Bw Okello.

Wafanyi kazi hao walizidi kuteta kuwa malipo ya mshahara ni duni na wakati mwingi huchelewa kutolewa, na ukiulizia kulipwa unapigwa bila huruma.

Mfanyi kazi mwingine Bw Francis Gaturu ambaye anafanya kazi katika afisi za kampuni hiyo alidhibitisha kuwa ni kweli wafanyi kazi wananyanyaswa lakini yeye pia kama mwajiriwa hana la kufanya bali yeye hubaki kujitazamia mambo na macho.

“Hata mimi nimeajiriwa miezi chache zilizopita na kwa hivyo bado najaribu kuelewa jinsi mambo yanavyoendeshwa eneo hili,” alisema Bw Gaturu.

Mfanyi kazi mwingine Bw Joseph Ndung’u Mwaura, pia ni mwingine ambaye hivi majuzi alidhulumiwa ambapo alitishwa hata kuachishwa kazi.

“Hapa kazi ni kuvumilia tu, cha muhimu ni kutafutia watoto chakula hayo mengine ni kuvumilia tu,” alisema Bw Mwaura.

Kutokana na masaibu hayo wafanyakazi hao kwa kauli moja wanaitaka serikali kuingilia kati ili kuwaokoa kutokana na mchina huyo ambaye amekuwa kero kwao.

Juhudi za kutaka kumhoji mmiliki wa kampuni hiyo ziligonga mwamba kwani hakutaka mazungumzo yoyote na waandishi wa habari.