Habari

Wachina 15 wafurushwa kwa kushiriki ukahaba South C

September 19th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

RAIA 15 wa Uchina wakiwemo wanawake 13 na wanaume wawili, Jumatano walikamatwa kwa madai ya kushiriki ukahaba jijini Nairobi huku serikali ikizidisha msako dhidi ya raia wa kigeni wanaoishi nchini kiharamu.

Idara ya Uhamiaji ilisema maafisa wake wakishirikiana na wale wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) waliwakamata Wachina hao katika mtaa wa South C asubuhi kwenye nyumba mbili zinazoaminika kuwa madanguro, wakafurushwa nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji, Bw Alexander Muteshi, alisema mmoja wao alikuwa amefurushwa nchini Mei 2017 kwa kuhusishwa na ukahaba na michezo haramu ya bahati nasibu lakini akarejea kwa kutumia paspoti tofauti.

“Tunashukuru mchango wa wawekezaji wa kigeni katika uchumi wa nchi hii lakini tunasisitiza kuwa wanaweza kufaidika tu kwa kufanya biashara halali nchini humu,” akasema.

Wakati huo huo, alisema idara yake ilizuilia Waganda 10 ambao walikuwa wanapelekwa Mashariki ya Kati na Mkenya ambaye anashukiwa kuwa mlanguzi wa binadamu katika mtaa wa Uhuru, Nairobi.Hivi majuzi, polisi walivamia makao makuu ya shirika la habari la China Global Television Network na kukamata wanahabari kadhaa wakiwemo Wachina 13 ambao walidhaniwa kuwa nchini bila idhini.

Baadhi ya Wachina waliokamatwa kwa danguro mtaani South C, Nairobi Septemba 19, 2018. Picha/ Hisani

Hata hivyo, waliachiliwa huru baada ya serikali kutambua kuwa habari zilizotolewa kuwahusu hazikuwa za kweli na Wachina hao walikuwa na vibali vinavyowaruhusu kufanya kazi Kenya kisheria.

Wakati huo, Ubalozi wa Uchina nchini ulisema taifa hilo linaheshimu sheria za Kenya lakini ikataka raia wake walio nchini kihalali wasidhulumiwe.

Raia mwingine wa Uchina, Bw Liu Jiaqi, alifurushwa nchini mapema mwezi huu baada ya video kufichuka ikimwonyesha akitoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya Wakenya akiwemo Rais Uhuru Kenyatta.

“Ubalozi wa Uchina nchini Kenya huhitaji kampuni zote za Uchina na watu binafsi wafuate sheria za nchi, waishi na kufanya kazi Kenya kwa msingi wa sheria,” taarifa ya ubalozi huo ikasema.

Ingawa serikali ilizidisha juhudi zake za kusaka na kufurusha raia wa kigeni walio nchini kiharamu mwaka huu, raia wengi wa Uchina wamewahi kukamatwa na kufurushwa kwa msingi huu kwa miaka kadhaa sasa, hasa baada ya ushirikiano kati ya Kenya na Uchina kushika kasi katika kipindi cha miaka michache iliyopita na kufanya raia wengi wa nchi hiyo kuja nchini sana sana kufanya kazi kwa ujenzi wa miradi mikubwa kama vile barabara na reli ya kisasa.

Ripoti zinaonyesha kuna raia wa kigeni ambao huja nchini kama watalii kisha kutafuta njia za kilaghai ili waanze kufanya kazi zisizoruhusiwa na sheria za Kenya.

Serikali ilikuwa imetoa nafasi kwa raia wa kigeni kuhakikisha wana stakabadhi zifaazo kuwa nchini na kipindi hicho kilikamilika karibu miezi miwili iliyopita.