Habari Mseto

Wachina 3 waliokamatwa na nyama zilizooza wazuiliwa

January 9th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA watatu wa Uchina waliotiwa nguvuni Januari 8, 2019 katika mtaa wa Kilimani wakiwa na nyama za wanyamapori zilizokuwa zimeoza wameagizwa wazuiliwe kwa muda wa siku tano kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi.

Hakimu mwandamizi aliamuru Shang Li Yan, Xing Wei, Zhang Jie na raia wa Kenya, Bw David Maseno Oseko wazuiliwe hadi Januari 14, 2019 katika kituo cha polisi cha Kilimani Nairobi.

Polisi walimweleza hakimu mkazi Bi Muthoni Nzibe kuwa washukiwa hao walikutwa wamehifadhi katika makazi yao bidhaa za wanyamapori pamoja na nyama zilizokuwa zinaendelea kuoza kwenye majokofu manne.

“Polisi watawashtaki washukiwa hawa kwa makosa mbalimbali ya kupatikana na ngozi ya chui na pembe za ndovu.”

Mahakama ilielezwa kuwa washukiwa hao walikuwa na bidhaa ambazo hazikuwa zimelipiwa ushuru.

Washukiwa hao walipofikishwa mbele ya hakimu mkazi Bi Nzibe, upande wa mashtaka uliomba upewe muda wa siku 10 kukamilisha uchunguzi na kuwafungulia mashtaka raia hao wa Uchina.

Hakimu alielezwa washukiwa hao wanadhaniwa kushirikiana na wawindaji haramu kushiriki uhalifu.

Washukiwa hao raia wa Uchina walitiwa mbaroni Januari 8 katika mtaa wa Kilimani, Kaunti ya Nairobi pamoja na mjakazi wao raia wa Kenya, Bw Yan.