Habari Mseto

Wachina 3 wanaswa wakiwa na bidhaa haramu za wanyamapori

January 9th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MAAFISA wa polisi kutoka kitengo cha DCI, Nairobi wanatarajiwa kuwafikisha kortini watu watatu raia wa China Jumatano, baada yao kukamatwa wakiwa na bidhaa haramu za wanyama wa porini.

Watatu hao walikamatwa katika mtaa wa Kilimani Jumanne katika jumba moja lililokuwa makazi yao, wakiwa na ngozi za chui, pembe za ndovu na kifaru na kobe aliye hai.

Idara ya DCI kupitia akaunti yake ya twitter ilisema Xing Wei, Zhang Jie na Shang Li pamoja na Mkenya David Maseno Oseko walifumaniwa wakiwa na bidhaa hizo, kabla ya kutiwa nguvuni.

“Raia watatu wa China- Xing Wei, Zhang Jie na Shang Li na Mkenya David Maseno Oseko leo (Jumanne) walikamatwa katika eneo la Kilimani na maafisa wa DCI wakiwa na bidhaa za porini kama ngozi ya chui, pembe za ndovu na kifaru na kobe aliye hai. Watafikishwa kortini Jumatano,” ikasema idara hiyo.