Habari MsetoVideo

Wachina wahukumiwa kufagia mahakama

June 13th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

RAIA watatu wa Uchina Ijumaa walisukumiwa kifungo cha kufanya kazi ya kufagia Mahakama baada ya kukiri walipatikana na bidhaa ambazo hawakuwa wamelipia ushuru wa forodha Sh14,000.

Washtakiwa hao walianza kufanya mara moja kazi ambayo haikuwaleta humu nchini. Walikuwa maafisa wa uuzaji bidhaa mbalimbali wa kampuni moja nchini Uchina.

Watatu hao Bi Emily Peng, Bw Lee Liang na Jason Shen waliadhibiwa na hakimu mkazi Bi Emily Mugure walipokiri shtaka dhidi yao.

Washtakiwa hao walimsihi Bi Mugure awaonee huruma na awasamehe kwa vile “walikuwa maajenti wa kampuni moja ya Uchina inayotengeneza nyaya za stima na kamwe hawakujua bidhaa walizokuwa nazo hazijalipwa ushuru.”

Peng, Liang na Shen  walisema walitumiwa vibaya lakini wakaomba korti isipige kwa fimbo ya chuma.

Watatu hao walikamatwa na maafisa wa mamlaka ya ushuru nchini KRA katika jengo la Jomo Kenyatta International Conference Centre (KICC) wakionyesha bidhaa mbali mbali zinazotengenezewa nchini Uchina, zinazoweza kupata soko humu nchini kwa bei nafuu.

Washtakiwa walikuwa na mafungu saba ya nyaya za umeme. Nyaya hizo hazikuwa zimelipiwa  ushuru wa Sh14,000 kwa KRA.

Walikiri walikutwa na nyaya hizo na bidhaa nyinginezo katika maonyesho KICC ya bidhaa mbali mbali.

“Tunaomba msamaha. Tulifika humu nchini Mei 29, 2018 tukiwa maajenti wa kampuni moja ya Uchina inayotengeneza nyaya za stima. Hatukujua chochote kuhusu ushuru wa forodha. Sisi ni wageni.Hatujui sheria za Kenya. Tulitumiwa vibaya na kampuni iliyotutuma kushiriki katika maonyesho KICC kusudi ipate soko ya bidhaa inazotengeneza,” walijitetea.

Pia walisema walishirikiana na maafisa wa KRA na Polisi waliowahoji. Akipitisha hukumu , Bi Mugure aliwaamuru washtakiwa wafagie korti hadi saa 11 alasiri kisha waachiliwe.

“Mtafagia mahakama mkisimamiwa na afisa wa hii korti hadi saa 11 kisha mwachiliwe,” aliamuru Bi Mugure huku akiwaonya wasirudie kosa kama hilo tena.

Aliwapa siku 14 kukata rufaa ikiwa hawakuridhika. Washtakiwa walitolewa kizimbani na kupelekwa seli ambapo walipewa kazi ya kufagia na kusafisha  korti.

Video Gallery